1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jinsi ya kuulinda udongo dhidi ya ukame

5 Desemba 2022

Udongo wenye rutuba ni muhimu kwa upatikanaji wa chakula duniani pamoja na maelfu ya spishi zinazoishi ardhini. Katika Siku ya Udongo Duniani, DW inaangalia kinachoweza kufanywa kuulinda udongo kutokana na ukame

https://p.dw.com/p/4KUkB
Symbolbild Erdboden
Picha: Florian Gaertner/photothek.net/picture alliance

Udongo unaweza tu kupuuzwa kama uchafu kwenye vyatu vyetu. Kitu ambacho hatukijali mno, isipokuwa kama wewe ni mtunza bustani au mkulima. Lakini kwa hakika ni muhimu sana kwa Maisha yetu. Kwa sababu bila ya udongo, kupanda chakula itakuwa tatizo.

Lizeth Vasconez Navas, mtafiti katika Taasisi ya Hamburg ya Sayansi ya Udongo anasema tunachoona sasa ni kuwa vipindi vya ukame vinakuwa vikali sana, na mmomonyoko wa udongo pia unakuwa mkubwa zaidi.

Kwa hiyo vipi tunaweza kulinda udongo?

Ili kuzuia udongo ulio kavu dhidi ya kutoweka kupitia mmomonyoko, watalaamu wanasema ni muhimu kupanda mimea upya haraka iwezekanavyo. Mimea inayokuwa kwa haraka inaweza kuzuia kutoweka kwa udongo wakati pia ukisaidia kurejesha virutubisho kwa kuongeza naitrojeni kwenye udongo.

Dürre in Angola
Ardhi kavu na yenye joto kali nchini AngolaPicha: OSVALDO SILVA/AFP

Haya mazao ya kufunika kama vile kunde, ngano, na shayiri yanaweza kutumika kama ngao ya asili, kwa kupunguza uvukizi na kuhifadhi unyevu wakati pia yakipunguza nyuzijoto ardhini.

Yanaweza kuboresha rutuba ya udongo kwa kipindi kirefu kwa kudhibiti mmomonyoko, kwa kukandamiza magugu na watutu, kuimarisha mifumo ya mizizi na kuongeza viumbe vai, kwa mujibu wa ripoti yam waka wa 2021 kutoka Baraza la Nishati, Mazingira na Maji, taasisi ya utafiti ya India.

Unyevu wa udongo pia ni muhimu kwa Wanyama waishiyo chini ya ardhi.

Nicole Wellbrock, mtalaamu wa udongo kutoka taasisi ya Thünen inayohusika na Mifumo ya Ikolojia ya Misitu, kaskazini mashariki mwa Berlin, anasema wakati udongo unapokuwa kavu na wa moto, vijidudu husitisha shughuli zao.

Kurudisha miti mashambani

Vasconez Navas wa Chuo Kikuu cha Hamburg anasema tunapaswa kuangalia nyuma kwenye mazingira ili kusaidia mifumo ikolojia na udongo kujitengeneza upya baada ya vipindi virefu vya matumizi ya kupitiliza. Mojawapo ya suluhisho ni kilimo mseto, ambapo miti hupandwa kwenye mashamba ya vyakula.

Italien Trockenheit
Wakulima wa mchele Italia wanakabiliwa na ukamePicha: Mauro Ujetto/NurPhoto/picture alliance

Wellbrock wa Taasisi ya Thünen anasema miti kwa ujumla haichanganyiki na mashamba ya wakulima katika maeneo kama Ujerumani. Anasema katika siku za nyuma, iliondolewa kama sehemu ya mageuzi ya kilimo, kwa sababu hiyo ilikuwa ardhi ya kilimo, na wakulima walipendelea maeneo makubwa na yanayofanana.

Miti haisaidii tu kudhibiti mmomonyoko na uvukizi na kutengeneza kivuli, pia inaweza kusaidia kuufufua udongo ulioharibiwa na ukame.

Spishi kadhaa za miti, inayofahamika kama miti ya mbolea, huchukua naitrojeni kutoka hewani na kuiweka udongoni kupitia mizizi na majani yanayoanguka.

Hii husaidia wakulima kuboresha rutuba ya ardhi kwa kutumia mbolea mbadala za viwandani za bei nafuu.

Nchini Malawi, Zambia, Burkina Faso na nchi nyingine za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika, miti hii inasaidia kuongeza mara dufu au mara tatu mazao ya mahindi, ambacho ni chakula muhimu.

Suluhisho za teknolojia ya chini

Katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania na Kenya, jamii zinatumia mbinu ya chini ya teknolojia kupambana na kuenea kwa jangwa.

Mbinu yao huhusisha kuchimba mitaro ambayo hukusanya maji wakati kunaponyesha, na kuyazuia kuyeyuka haraka kutoka kwenye udongo ulioungua. Mbegu za nyasi kisha hupandwa kwenye mitaro hiyo ambazo huota, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kupunguza kiwango cha nyuzi joto ardhini.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Iddi Ssessanga