1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan: Tulimkamata waziri mkuu kwa usalama wake

Sylvia Mwehozi
26 Oktoba 2021

Jenerali wa kijeshi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan, amesema waziri mkuu Abdalla Hamdok aliyekamatwa Jumatatu na maafisa wengine anashikiliwa nyumbani kwa kamanda huyo na sio jela na kwamba yuko katika afya njema. 

https://p.dw.com/p/42CzU
Sudan General Abdel Fattah al-Burhan
Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametetea hatua ya jeshi kutwaa madaraka kwamba ilikuwa ya lazima ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe. Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu alipotangaza kudhibiti madaraka, al-Burhan amewashutumu wanasiasa kwa uchochezi dhidi ya vikosi vya usalama. Amedai kwamba Hamdok anashikiliwa nyumbani kwake na hajadhurika hata kidogo. Kiongozi huyo wa kijeshi anasema kitendo hicho cha jeshi hakiwezi kuhesabiwa kama mapinduzi kwasababu jeshi lilikuwa likijaribu kurekebisha njia ya kipindi cha mpito cha kisiasa.

"Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alikuwa nyumbani kwake, lakini tuliogopa angedhurika, sasa anakaa nyumbani kwangu, tulikuwa tumekaa pamoja jana jioni, na anaendelea na maisha yake kawaida. Atarudi nyumbani mzozo utakapokwisha na vitisho vyote vikiisha, lakini kwa sasa anakaa nami nyumbani kwangu."Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuijadili Sudan

Katika hatua nyingine, kamanda huyo amependekeza kwamba baadhi ya maafisa wa serikali iliyovunjwa wanaweza kukabiliwa na mashtaka lakini akaongeza kwamba waziri mkuu anashikiliwa kwa ajili ya usalama wake na huenda akaachiwa hivi karibuni.

Sudan Putsch Protest Ausschreitungen
Vizuizi vilivyowekwa barabarani na waandamanajiPicha: AFP/Getty Images

Wakati huohuo waziri wa mambo ya nje katika serikali iliyovunjwa Mariam al-Mahdi, ameonekana kukaidi tangazo la jeshi na kusema yeye na baadhi ya wanachama wengine katika utawala wa Hamdok ndio wenye mamlaka halali nchini Sudan.

Waziri huyo amelieleza shirika la habari la Associated Press kwa njia ya simu kuwa "Bado tuko katika nafasi zetu. Tunakataa mapinduzi kama hayo na hatua zilizo kinyume na katiba. Tutaendelea kutotii sheria kwa njia za amani na upinzani ".

Hayo yakijiri Mabalozi watatu wa Sudan barani Ulaya wametangaza kujitenga na watawala wa kijeshi na kulaani mapinduzi ya yaliyotokea na kuarifu kwamba balozi zake hivi sasa ziko mikononi mwa Wasudani. Taarifa hiyo imetolewa na wizara ya habari na utamaduni, na kuwataja mabalozi hao kuwa waliokuwa wakiiwakilisha Sudan katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Uswisi.

Afisa katika wizara ya afya alisema kwamba watu saba wameuwawa katika machafuko yaliyozuka baina ya waandamanaji na vikosi vya usalama siku ya Jumatatu. Hadi kufikia leo Jumanne maisha katika mji mkuu wa Khartoum yalikuwa kama yamesimama na mji pacha wa omdurman, huku maduka yakiwa yamefungwa na miali ya moshi ikichomoza kutoka eneo walipo waandamanaji wanapochoma matairi.