1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema imemuuwa kiongozi wa Hezbollah, Nasrallah

28 Septemba 2024

Jeshi la Israel limesema limemuuwa Hassan Nasrallah, kiongozi wa kundi la Hezbollah, nchini Lebanon. Nasrallah aliuliwa katika shambulio la Israel kwenye kitongoji cha Beirut usiku wa kuamkia Jumamosi.

https://p.dw.com/p/4lBsq
Mwanamke akiwa ameshika picha ya kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah
Mwanamke akiwa ameshika picha ya kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah Picha: Vahid Salemi/picture alliance/AP

Hezbollah hadi sasa haijathibitisha kifo cha Nasrallah.

Lakini jeshi la Israel kupitia mtandao wake wa X limesema Hassan Nasrallah hatoweza tena kuutishia ulimwengu.

Taarifa ya jeshi la Israel imesema kuwa Ali Karaki kamanda wa Hezbollah anayehusika na kusini mwa Lebanon, pia aliuawa. 

Hofu kwamba mashambulizi kati ya Israel na Hezbollah yanaweza kuongezeka na kuwa vita kamili imeshika kasi tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi kuyalenga makao makuu na ngome za Hezbollah. 

Lebanon imesema mashambulizi ya Isreal toka Jumatatu yamewauwa mamia ya watu.

Kuuawa kwa Nasrallah, mwenye umri wa miaka 64, ambaye amekuwa akiliongoza kundi lenye nguvu la Hezbollah, lenye makao yake nchini Lebanon kwa miaka 30, itakuwa pigo kubwa kwa kundi hilo.