Wanajeshi wa Israel wavamia hospitali katika ukanda wa Gaza
16 Novemba 2023Baada ya wanajeshi wa Israel wa kufanya upekuzi wa saa kadhaa katika hospitali ya Al-Shifa katika ukanda wa Gaza, jeshi hilo limedai kupata vifaa vya kijeshi ndani ya majengo ya hospitali hiyo. Israel imekuwa ikiyatoa madai hayo kwa siku kadhaa sasa ikisema kundi la Hamas linatumia majengo ya hospitali hiyo kama kamandi yake na eneo la maficho ya silaha. Taarifa za kukutwa silaha zilipingwa mara moja na Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza.
Taswira tofauti zatolewa kuhusu uvamizi wa majengo ya hospitali
Kuhusu tukio lenyewe la uvamizi wa majengo ya hospitali, kila upande umetoa taswira tofauti ya kilichotokea.
Israel imechapisha mkanda wa vidio ulioonesha wanajeshi wake wakisaidia kubeba makasha yenye maandishi yaliyosomeka "chakula cha watoto" na mengine "vifaa tiba" katika kile ilichotaka kuonesha kwamba msako wake ndani ya hospitali hiyo haukuzusha taharuki na wanajeshi hawakuwa kitisho.
Soma pia:Uvamizi wa Israel katika hospitali ya Gaza wazusha wasiwasi wa kimataifa
Hata hivyo mamlaka za Ukanda wa Gaza zimeelezea hali tofauti kabisa. Zimesema wafanyakazi na watu waliokuwemo kwenye hospitali hiyo walijawa hofu wakati wote wa msako wa jeshi la Israel.
Wanajeshi wa Israel wafanya upekuzi mkali
Shirika la Habari la Associated Press limearifu kwamba msako huo ulipoanza wanajeshi wa Israel waliamuru vijana wote mabarobaro kujisalimisha, wakatolewa nje ya majengo ya hospitali na kufanyiwa upekuzi mkali wengine wakiwa bila nguo.
Mwandishi habari wa shirika moja la kimataifa aliye miongoni mwa watu waliokwama kwenye hospitali hiyo, amesema vikosi vya Israel vilifanya upekuzi kwenye kila chumba.
Jeshi la israel ladai kupata silaha na vifaa vya kijeshi katika majengo ya hospitali
Msako huo ulimalizika majira ya jioni kwa taarifa ya jeshi la Israel kusema askari wake wamekuta silaha, nyaraka za ujasusi na vifaa vya kijeshi. Wamedai pia wamevikuta vifaa vya mawasiliano vyenye kuashiria kwamba eneo hilo ndiyo yalikuwa makao makuu ya mawasiliano ya kundi la Hamas.
Soma pia:Ukingo wa Magharibi: Vurugu za Waisrael zaongezeka dhidi ya Wapalestina
Jeshi la Israel limechapisha vilevile taarifa zinazonesha bunduki, maguruneti na vifaa vingine inavyodai kuwa imevikuta ndani ya hospitali. Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imekanusha madai hayo ikisema "vikosi vya Israel havikukuta vifaa vyovyote vya kijeshi wala silaha ndani ya hospitali."
Taarifa ya Munir al-Bursh afisa wa ngazi ya juu wa wizara hiyo ya afya amesema chini ya misingi ya uendeshaji hospitali hakuna silaha zinazoruhusiwa.
Wizara ya afya ya ukanda wa Gaza yawatuhumu wanajeshi wa Israel kwa uharibifu
Wizara hiyo ya Afya imewatuhumu wanajeshi wa Israel kwa kuharibu vifaa vya matibabu inavyosema havipatikani kokote ndani ya ukanda wa Gaza.
Pia imesema Israel imewakamata wahandisi wawili waliokuwa wakifanya kazi ndani ya hospitali hiyo kwenye usambazaji wa umeme na hewa ya oksijeni inayotumiwa na wagonjwa.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa latoa wito wa kurefushwa usitishaji mapigano katika ukanda wa Gaza
Katika hatua nyingine Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa "kurefushwa kwa usitishaji mapigano" chini ya misingi ya kiutu kwenye mzozo wa Ukanda wa Gaza. Hiyo ni mara ya kwanza kwa baraza hilo lenye jukumu la kusimamia amani ya ulimwengu kuvunja ukimya tangu kuanza kwa mzozo mbaya kabisa kati ya Israel na kundi la Hamas.
Soma pia:Vifaru vya Israel vipo kwenye milango ya hospitali ya Gaza
Kwenye kikao cha Jumatano jioni, baraza hilo limepitisha azimio lililoandaliwa na Malta na kupata uungaji mkono wa wanachama 12 wengine. Marekani, Uingereza na Urusi zilijizuia kulipigia kura azimio hilo lililofikishwa mbele ya baraza la usalama lenye nchi 15 wanachama. Karibu kila aya ya azimio hilo limewataja watoto hususani likitaka "pande zote kuheshimu sheria ya kimataifa kuwalinda raia, hasa hasa watoto".