1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifaru vya Israel vipo kwenye milango ya hospitali ya Gaza

14 Novemba 2023

Vikosi vya Israel vimeshambulia kusini mwa Gaza baada ya vifaru kusonga mbele kwenye milango ya hospitali kubwa kabisa iliyozingirwa katika upande wa kaskazini ya Al-Shifa

https://p.dw.com/p/4YmJa
Gazastreifen IDF rückt weiter auf Gaza-Stadt vor
Picha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Takribani watu 13 wameuawa baada ya vikosi vya Israel kuyalenga makazi yao katika mji wa kusini wa Khan Younis. Maafisa wa wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza wamesema jeshi la Israel pia limeviweka vifaru nje ya hospitali ya Al Shifa, ambayo ndio kituo kikuu cha matibabu katika jiji la Gaza, na ambacho Israel inasema chini yake kuna mahandaki yanayotumika kama makao makuu ya wapiganaji wa Hamas wanaotumia wagonjwa kama ngao. Hamas inakanusha madai hayo.

Soma pia: Uhaba wa mafuta watatiza shughuli za kiutu Gaza

Israel imesema inasimamia utaratibu wa kupelekwa Gaza mashine za kuwatunza watoto njiti, katika hatua ya kuwezesha kuhamishwa watoto wachanga kutoka hospitali hiyo.

Msemaji wa wizara ya afya ya Gaza Ashraf Al-Qidra ambaye alikuwa ndani ya hospitali ya Al Shifa, amesema jana kuwa wagonjwa 32 walifariki dunia katika siku tatu zilizopita, wakiwemo watoto watatu wachanga. Kwa sasa kuna wagonjwa 650 ndani ya hospitali hiyo. Mkurugenzi wa hospitali ya Al-Shufa Mohammad Abu Salmiyah amesema watu 179, wakiwemo watoto na wagonjwa waliofariki katika kitengo cha wagonjwa mahututi, wamezikwa kwenye kaburi la pamoja hospitalini hapo.

Hospitali ya Al-Shifa ndio kubwa kabisa katika Ukanda wa Gaza
Wagonjwa 650 wamelazwa katika hospitali ya Al-ShifaPicha: Khader Al Zanoun/AFP

Soma pia: Hosptali kubwa ya Gaza yakabiliwa na mashambulizi ya karibu

Katika matamshi yake ya kwanza tangu kuripotiwa kwa vifo vya wagongwa katika hospitali ya Al Shifa, Rais wa Marekani Joe Biden alisema hospitali lazima zilindwe.

Machafuko ya Ukingo wa Magharibi

Kundi la kijeshi la Hamas linalofahamika kama Al-Qassam Brigades linasema liko tayari kuwaachia hadi wanawake na Watoto 70 wanaoshikiliwa Gaza, kwa kubadilishana na usitishwaji mapigano kwa siku saba katika vita hivyo.

Msemaji wa Al-Qassam Abu Ubaida amesema waliwaambia wapatanishi wa mzozo huo, Qatar kuwa wanaweza kuwaachia huru mateka 50 hadi 70 kutokana na ugumu kuwa wanashikiliwa na makundi tofauti. Israel ambayo imeizingira Gaza, imekataa mpango wa usitishwaji kamili wa mapigano, ikihoji kuwa Hamas inaweza kutumia fursa hiyo kujipanga upya, lakini imeruhusu usitishwaji vita kwa nyakati Fulani kwa misingi ya kiutu, ili kuruhusu chakula na bidhaa nyingine kuingia Gaza na kuondoka kwa raia wa kigeni.

Katika Ukingo unaokaliwa wa Magharibi, karibu Wapalestina wanane wameuawa na vikosi vya Israel. Wizara ya Afya ya Palestina na vyombo vya Habari vya Palestina vimesema watatu kati ya hao waliuliwa katika shambulizi la droni ya Israel. Jeshi la Israel na polisi wamesema vikosi vyao vilivyotumwa katika eneo la Tulkarm kuwakamata washukiwa wa kigaidi, walishambuliwa na wakawauwa wapiganaji wa Kipalestina katika vurugu zilizozuka.

Wakati huo huo, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinaadamu – OCHA imesema watu wengine 200,000 wamekimbia kaskazini mwa Gaza tangu Novemba 5.

afp, ap, dpa, reuters