Jeshi la DRC lapambana na M23 Kivu Kaskazini
7 Februari 2024Mji wa Goma ulishambuliwa kwa mabomu asubuhi ya Jumatano (Februari 7) tukio lililosababisha hofu kwa wakaazi wa mji huo.
Taarifa zaidi zilifahamisha kwamba milio ya risasi iliendelea kusikika kwenye vijiji vya Kiuli na Malehe vilivyo umbali wa kilomita 7 kutoka mji wa Sake, ambako waasi wamezishambulia kwa mizinga ngome za jeshi la Kongo.
Soma zaidi: Takriban raia 20 wauawa kwenye shambulizi nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo
Kutokana na hofu, raia katika mji wa Sake wameanza kuukimbia mji huo.
Vyanzo vya ndani vilieleza kuwa mabomu mawili ya wapiganaji wa M23 yaliyorushwa kutokea eneo la Misekera yalianguka karibu na kambi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) kwenye milima ya Kihuli, nje kidogo ya mji wa Sake ambako pia raia wameanza kukimbia.
Hata hivyo, kwenye barabara ya Shasha hali ilikuwa imeanza kuwa tulivu baada ya wapiganaji wajiitao "Wazalendo" kuwafurusha waasi wa M23.