Jerusalem. Chama kinachowawakilisha Wayahudi walowezi kimesema kuwa hatua ya serikali ya kujiondoa katika eneo la Gaza inaweza kuleta vita vya wenyewe kwa wenyewe.
29 Machi 2005Matangazo
Walowezi wa Kiyahudi wameapa kufanya maandamano dhidi ya hatua ya serikali ya Israel ya kujiondoa katika eneo la Gaza. Chama kinachowawakilisha walowezi hao cha Yesha kimetoa onyo kuwa hatua hiyo inaweza kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuongeza kuwa kiasi cha watu 100 000 wataandamana katika maeneo hayo yaliyopangwa kuhamishwa wakaazi wake.
Bunge la Israel linatarajiwa kupitisha bajeti ya taifa baadaye leo katika hatua nyingine kuelekea kuidhinisha mpango huo wa kujiondoa. Jana bunge lilitupilia mbali muswada unaotaka kufanyike kura ya maoni kuhusiana na suala la mpango huo wa kujiondoa kutoka Gaza hali ambayo ingechelewesha mpango huo. Hatua hiyo ya kujiondoa kwa Israel katika maeneo ya Gaza kunatarajiwa kuanza mwezi Julai.