Je uchaguzi utakuwa wa huru na haki Uganda?
8 Januari 2021Joto la uchaguzi nchini Uganda linahisika kila mahala kutokana na matamshi ya wanasiasa pamoja na askari wa jeshi na polisi wanaonekana kila mahala wakiwa wamejihami kama ambao wanaelekea vitani.
Wananchi wenyewe wanaonekana kujiandaa kwa hali ambayo wengi wanabashiri itakuwa ya mshikemshike katika uchaguzi huu na wanachoelezea kuhofia zaidi ni vurugu na machafuko.
Sheikh Abdallah Sabiila ambaye ni Kadhi wa kanda ya Sebei amesema vyombo vya dola vimetumiwa kupindukia kukandamiza hasa upinzani. Na upinzani umejaribu kukabiliana nao kulinda maslahi yao na kwa hiyo patakuwa na mapambano kwa sababu kuna msemo kuwa mgombea wa NRM lazima ashinde kwa vyovyote.
Upinzani waulaumu utawala wa Rais Museveni kwa hali ya taharuki nchini Uganda.
Viongozi wa upinzani wana mtazamo kuwa utawala wa Rais Museveni ndiyo ulaumiwe kwa hali hii ya taharuki iliyotandaa na kuwasababisha wananchi kuingiwa na hofu.
"Uchaguzi usichukuliwe kuwa vita ili tutazamane kama watu walio katika uwanja wa vita kwani majeshi yamedhibiti kila suala la uchaguzi huo na kwa hiyo hauwezi kuwa huru na wa haki," alisema Winnie Kiiza mratibu wa kampeni wa chama cha ANT
soma zaidi: Wanaharakati wa haki za binaadamu wahofia usalama wao Uganda
Kinachoshangaza ni kwamba hata Rais Museveni mwenyewe anashuku kwamba kuna njama za udanganyifu kufanyika ili kumsababisha asishinde katika uchaguzi huu. Museveni amesema kuna watu wanaopanga kuiba kura ikiwemo maafisa wa uchaguzi ambao watapewa rushwa kubadili matokeo.
Lakini msemaji wa chama cha upinzani cha FDC, Ibrahim Semujju, amemtaka Rais Museveni akubali matokeo ya uchaguzi endapo atashindwa na aoneshe uzalendo kwa kukabidhi madaraka kwa amani. La sivyo itaamamisha kuwa yeye hajali kama nchi itatumbukia katika hali ya suintofahamu.
Ikumbukwe kuwa mwaka 1980, Museveni ndiye alitumbukiza Uganda katika suintofahamu iliyodumu miaka mitano na kusababisha vifo vya mamia ya watu pale alipopinga matokeo ya uchaguzi na kuanzisha harakati za kumwondoa rais aliyetangazwa mshindi, Milton Obote.
Wakati huo huo, Upinzani na baadhi ya wagombea kwa upande wa utawala aidha wameikosoa Tume ya Uchaguzi kwa kanuni mpya ambazo imetoa.
soma zaidi: Uganda: Upinzani wazindua jukwaa la kufuatilia uchaguzi
Tume hiyo imetishia kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi ya kituo chochote ambapo watu watakataa kuondoka baada ya kupiga kura na pia hakuna mtu atakubaliwa kwenda na simu kwenye vituo hivyo.
Wadau wanaelezea kuwa simu zitasaidia katika kuwasilisha na hata kuhifadhi ushahidi wa vitendo vyovyote vitavyoweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.
Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala