1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakatiwa haki za binaadamu wahofia usalama wao Uganda

7 Januari 2021

Wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na wanasheria wamelezea hofu na mashaka kuhusu usalama wao huku mgombea urais Robert Kyagulanyi akisema amewahamishia Marekani watoto wake kufuatia vitisho vya usalama

https://p.dw.com/p/3ndvs
Uganda Polizei vor dem Haus von Bobin Wine
Picha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Visa vya wanaharakati wa haki za binadamu na wanasheria kukamatwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu vimewatia wadau katika jumuiya hiyo katika wasiwasi kwamba utawala wa sasa unawalenga kwa kuwa wanachunguza vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mwezi uliopita jaribio la asasi za kiraia kuanzisha elimu ya kuwahamasisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika uchaguzi zilikwama pale pesa za makundi hayo zilipofungiwa katika benki kufuatia agizo la serikali.

Mwanasheria Nicholas Opiyo ambaye alikuwa ameanzisha mchakato wa kuwasilisha rufaa kupinga hatua hiyo baadaye mwenyewe alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya utakatishaji fedha.

Kulingana na rais wa jumuiya ya wanasheria nchini, Pheona Wall wanahseria wengine kadhaa wamekamatwa katika mazingiraya kutatanisha na hata wengine kudai kupokea vitisho kutoka kwa watu wasiowajua kupitia kwa ujumbe wa simu. Jumuiya hiyo sasa iko njiapanda, isijue nani atawalinda wao ambao hupigania haki za binadamu.

Bobi Wine aihamishia familia yake nchini Marekani

Uganda Kampala Oppositioneller Bobi Wine
Mgombea wa Urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu aka Bobi WinePicha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Mwanaharakati mashuhuri wa  haki za binadamu Margaret Sekkaja ameeleza kuwa katika kipindi hiki wanakabiliwa na wakati mgumu kuhakikisha kuwa haki za binadamu hazikiukwi kwa sababu vyombo vya usalama vimejihusisha mno katika siasa na uchaguzi wa mara hii.

Vitisho na mashaka kuhusu hali itakavyokuwa katika uchaguzi mkuu pia vimemlazimu mgombea urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine kuwahamisha watoto wake hadi Marekani.

Ijapokuwa kuna maoni mbalimbali ya kuunga mkono maamuzi hayo kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wamemshtumu mgombea huyo. 

Lakini waziri wa nchi wa masuala ya kigeni OkolleOryem amekanusha kuwa utawala unawandama familia ya Bobi Wine.

Mgombea huyo aidha amendelea kukabiliwa na wakati mgumu kufuatia kukamatwa tena kwa timu yake ya kampeni alipokuwa akitokea mashariki mwa nchi.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala