Je Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh ni nani?
31 Julai 2024Wengi walimchukulia Haniyeh kuwa mtu wa misimamo ya wastani zaidi kinyume na wanachama wenzake wa Hamas ndani ya Gaza. Akiwa amezaliwa kwenye kambi ya wakimbizi na wazazi waliolazimika kukimbia makaazi yao kutokana na kampeni ya safisha safisha ya Israel, Haniyeh alianza harakati za kisiasa tangu akiwa mwanafunzi kwenye Chuo Kikuu cha Gaza, ambako alijiunga na kundi la Hamas lilipoundwa kwenye kile kifahamikacho kama Intifadha ya Kwanza ya 1987. Kwenye maisha yake amekamatwa na kufungwa jela mara kadhaa na hata kufukuzwa na kulazimika kuhamia nje ya nchi.
Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh auwawa Iran
Haniyeh alikuwa mwandani wa muasisi wa Hamas, Sheikh Ahmad Yasin, ambaye kama ilivyokuwa familia ya Haniyeh naye alikuwa mkimbizi kutoka kijiji cha Al Jura, karibu na Ashkelon. Mnamo mwaka 1994, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Yasin alikuwa kigezo cha kuigwa na vijana wa Kipalestina, akisema na hapa namnukuu: "Tulijifunza kutoka kwake mapenzi ya Uislamu na kujitowa kwa ajili ya Uislamu na kutokusalimu amri mbele ya maadui na vibaraka." Mwisho wa kumnukuu.
Kufika mwaka 2003, Haniyeh alikuwa msaidizi anayeaminika sana na Yasin na muda wote akionekana karibu na muasisi huyo wa Hamas hadi alipouawa na Israel mwaka 2004. Haniyeh alikuwa mmoja wapo wa watu wa mwanzo kuunga mkono wazo la Hamas kuingia kwenye siasa. Mwaka 1994, alisema kuunda chama cha siasa kungeliiwezesha Hamad kuyakabili mambo yanayojitokeza kwa ufanisi zaidi. Wazo hili kwanza lilikataliwa lakini baadaye likakubaliwa na uongozi wa Hamas na Haniyeh akaja akawa waziri mkuu wa Palestina baada ya Hamas kushinda uchaguzi wa mwaka 2006 na kuanza kuendesha serikali mwaka 2007.
Haniyeh alikuwa kipenzi na pia adui kwa wengi ndani na nje ya Palestina
Tangu mwaka 2017 alipoteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas, Haniyeh alikuwa daima yuko safarini baina ya Uturuki, Qatar, Misri na Iran, akitekeleza jukumu lake kama kiongozi mkuu wa ujumbe wa majadiliano na Israel wakati wa vita au mpigaji kampeni ya kimataifa kwa ajili ya Wapalestina wakati wa amani. Alikuwa kipenzi na pia adui kwa wengi ndani na nje ya Palestina. Baadhi ya mataifa yenye nguvu ya Kiarabu yalikuwa yanamchukulia kama mtu mkorofi.
Muda mfupi baada ya wapiganaji wa Hamas kulivamia eneo la kusini mwa Israel mnamo tarehe 7 Oktoba, Haniyeh alijitokeza kwenye kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kuyaonya mataifa ya Kiarabu yaliyokuwa yamerejesha uhusiano na Israel, akisema: "Makubaliano yote ambayo nyinyi mataifa ya Kiarabu mumesaini na Israel hayataweza kuumaliza mgogoro huu."
Washirika wa Hamas walaani mauaji ya kiongozi wake
Kabla ya kuuawa kwake, Haniyeh amepoteza ndani ya mwaka huu watoto wake watatu wa kiume - Hazem, Amir na Mohammad - baada ya gari yao kushambuliwa na kombora na Israel tarehe 10 Aprili. Kwenye mashambulizi hayo, wajukuu wanne wa Haniyeh pia waliuawa - wasichana watatu na mvulana mmoja.
Daima, Haniyeh alikanusha kwamba watoto wake walikuwa wapiganaji, lakini alipouliwa ikiwa mauaji hayo yangeliathiri mazungumzo anayoyaongoza ya kusaka amani ya Wapalestina, alisema na hapa namnukuu: "Maslahi ya watu wa Palestina yako mbele ya kila kitu."
Israel inauchukulia uongozi mzima wa Hamas kuwa magaidi na imewatuhumu Haniyeh na Meshaal na wengine kwa kuendelea "kushika hatamu za kundi la kigaidi la Hamas." Hadi alipouawa usiku wa kuamkia jana, haikuwa inafahamika ni kwa kiwango gani Haniyeh mwenyewe alijuwa kuhusu mashambulizi ya Oktoba 7 kabla ya kufanyika kwake, maana ulikuwa mpango wa siri sana hata kwa walioko Gaza kwenyewe.