Je Afrika yaweza kuimarisha demokrasia mwaka 2023?
27 Desemba 2022Nchi 17 za Afrika Ikiwemo Nigeria, Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zitafanya chaguzi kuu au za bunge mwaka wa 2023. Kulingana na kitengo cha Intelijensia kuhusu Uchumi, chaguzi hizo zitaliathiri bara hilo kwa kiasi kikubwa.
Kitengo hicho kimetahadharisha kwamba kipindi cha uchaguzi huweza kuandamwa na machafuko, na kwamba kuna hatari kubwa ya kuzuka kwa maandamano ya kisiasa na migomo katika nchi kadhaa.
Fonteh Akum, mkurugenzi mtendaji katika taasisi ya masomo ya kiusalama, alitaja majaribio ya hivi karibuni ya mapinduzi kule Sao Tome na Principe na kuliambia shirika la habari la DW kwamba:
Je mapinduzi yatakwisha mwaka 2023?
"Mwanzo kabisa kinachosubiriwa ni kuona ikiwa visa vya mapinduzi ambavyo vimeshuhudiwa barani humo mwaka 2022 vitaendelea au vitakomeshwa mwaka ujao. "
Nigeria, taifa linaloongoza barani Afrika kwa idadi kubwa ya watu, tayari imekumbwa na wimbi la machafuko ya kisiasa kuelekea uchaguzi wao mkuu wa mwezi Februari
Uchaguzi wa nchi hiyo ni muhimu kwa sababu ni kati ya nchi zinazoongoza kiuchumi lakini vilevile imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiusalama
Idadi kubwa ya vijana wapiga kura wanaoweza kuamua nani mshindi kati ya vyama vikuu nchini humo, pia ni jambo la kuzingatiwa.
Alex Vines ambaye ni mkuu wa miradi ya Africa katika taasisi ya wachambuzi Chatham House iliyoko mjini London pia amesema swali moja linalosalia ni ikiwa demokrasia itaimarishwa au itadhoofishwa kupitia chaguzi hizo barani Afrika.
"Chaguzi muhimu za kufuatiliwa kwa karibu ni nchini Nigeria, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zimbabwe, huku ikitabiriwa huenda zitakumbwa na machafuko."
Mashafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatarajiwa kufanya uchaguzi wake Disemba 20, mwaka 2023. Lakini machafuko yanayoshuhudiwa mashariki mwa Congo yanasababisha wasiwasi.
Kulingana na Akum, maamuzi ya rais Felix Tshisekedi kuhusu namna ya kushughulikia machafuko ya wanamgambo eneo hilo, yanaweza kuathiri uchaguzi huo.
Tshisekedi anatarajiwa kuwania tena urais na atapambana na mwansiasa wa upinzani Martin Fayulu.
Mivutano ya kisiasa Afrika Kusini
Nchini Afrika Kusini, chama tawala ANC ambacho kimeitawala nchi hiyo tangu mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, kilimchagua Rais Cyril Ramaphosa mwishoni mwa Disemba kuwa kiongozi na mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ramaphosa ambaye ametuhumiwa kushiriki utakatishaji wa fedha na ufisadi alikuwa akishinikizwa na upinzani ili ajiuzulu.
Chama hicho kiko njia panda huku nafasi yake ya kutwaa ushindi moja kwa moja ikitajwa kuwa hatarini.
Wachambuzi wa kisiasa wamesema cha kulaumiwa ni mika mingi ya utawala mbaya, sera kinzani na ufisadi kwa kiwango kikubwa.
Taarifa hii iliandikwa mwanzo kwa Kijerumani, kisha kimatafsiriwa kwa Kiingereza kisha hatimaye kwa Kiswahili.
Mwandishi: Martina Schwikowski