Janga la Mpox kuongeza mzigo wa gharama kwa nchi za Afrika
28 Agosti 2024Kuenea haraka kwa maambukizi ya virusi vya Mpox kusini mwa Jangwa la Sahara kunaweza kuziongezea nchi za sehemu hiyo mzigo mwingine wa gharama ambazo tayari zimebanwa kifedha. Shirika la kutathmini viwango vya uwezo wa kifedha, Fitch, limetahadharisha hayo.
Maradhi hayo ya hatari kubwa yalitangazwa na Shirika la Afya Duniani WHO, kuwa dharura ya afya kimataifa. Maambukizi ya Mpox yalilipuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuenea kwenye nchi jirani. Shirika la Fitch limesema milipuko ya maambukizi ya virusi hivyo vya mpox inaweza kusababisha athari kubwa za kiuchumi na kifedha, hata hivyo limesema athari hizo zinaweza kupunguzwa kwa ufadhili wa mataifa tajiri.
Fitch imezitaja Ivory Coast, Kenya, Rwanda, Afrika Kusini na Uganda kuwa ni miongoni mwa nchi zilizoripoti kuwa na watu wachache walioambukizwa mpox.
Hata hivyo, shirika hilo limesema kuna uwezekano kuwa baadhi ya nchi zinatoa orodha ya chini ya watu walioambukizwa. Nchi 13 za Afrika zimeorodhesha zaidi ya maambukizi 22,800 ya mpox na vifo 622 mwaka huu, kwa mujibu wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika.