1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la COVID lawatumbukiza wengi katika umasikini duniani

13 Aprili 2022

Umoja wa Mataifa umesema janga la corona liliwatumbukiza watu milioni 77 duniani katika umaskini na uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea hauwezi kurudi katika kiwango chake cha kawaida kutokana na gharama ya kulipa madeni

https://p.dw.com/p/49soO
Bildergalerie Brasilien Coronavirus | Reportage Jonathan Alpeyrie | Rio de Janeiro
Picha: Jonathan Alpeyrie

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ni ya kufadhili malengo ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 ikiwemo kumaliza umaskini, kuhakikisha kwamba vijana wote wanapata elimu na lengo la usawa wa kijinsia linaafikiwa.

Ripoti hiyo inasema mataifa tajiri yanaweza kurudia hali ya kawaida kutoka kwenye athari za janga la virusi vya corona kwa kuwa zilichukua mikopo yao kwa riba ya chini lakini nchi maskini zilitumia mabilioni ya dola kulipa madeni yao na madeni hayo yalikuwa kiwango cha juu cha riba. Hali hii ilizifanya nchi hizo kutoimarisha elimu, mifumo ya afya na uhifadhi wa mazingira.

soma zaidi: Athari za Covid miaka miwili baada ya kutangazwa kuwa janga

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mwaka 2019, kulikuwa na watu milioni 812 waliokuwa wakiishi katika umaskini na kufikia mwaka 2021 idadi hiyo iliongezeka na kufikia watu milioni 889.

Vita vya Ukraine pia vina athari kubwa kwa dunia

Äthiopien UN-Untergeneralsekretärin Amina Mohammed in Addis Abeba
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed Picha: Solomon Muchie/DW

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed katika mkutano na waandishi wa habari amesema vita vinavyoendelea nchini Ukraine vinaiathiri dunia kwa ujumla. Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 1.7  wanakabiliwa na gharama inayoongezeka ya vyakula, nishati na mbolea kutokana na vita vya Ukraine. Mohammed anadai vita hivyo vitazidisha hali kuwa ngumu duniani.

Maambukizi ya corona yaongezeka duniani

Naibu katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa litakuwa ni janga iwapo mataifa tajiri duniani yataongeza matumizi yao ya kijeshi kutokana na vita vya Ukraine na kupunguza misaada kwa mataifa yanayoendelea na kupunguza juhudi za kukabiliana na mizozo ya kimazingira.

Amesema kabla janga la virusi vya corona, umoja huo tayari ulikuwa nyuma katika juhudi za kuyatimiza malengo yake na vita vya Ukraine vitalemaza kabisa juhudi hizo kwa mara nyengine kwa hiyo anadai Umoja wa Mataifa unahitaji raslimali zaidi.

Ripoti hiyo inapendekeza kusamehewa madeni kwa nchi zinazokuwa kiuchumi, kuurekebisha mfumo wa kodi wa kimataifa kuhakikisha usawa katika usambazaji wa chanjo za virusi vya corona, kuzidisha kasi ya uekezaji katika nishati endelevu na kuboresha ushirikishwaji wa taarifa baina ya mataifa.

Chanzo: AP