Israel yasema imeyashambulia maeneo 100 ya Hamas huko Gaza
5 Januari 2025Jeshi la Israel limesema leo kwamba limeshambulia zaidi ya maeneo 100 yanayotumika kwa ugaidi katika Ukanda wa Gaza katika muda wa siku mbili zilizopita, huku waokoaji kwenye maeneo ya mamlaka ya ndani ya Palestina wameripoti makumi ya watu waliouawa katika mashambulizi hayo ya Israel.
Taarifa hiyo ya kijeshi imesema mashambulizi kadhaa yalilenga maeneo ambayo wanamgambo wa Kipalestina walikuwa wakirusha makombora kuelekea Israel katika siku za hivi karibuni na kwamba wamefanikiwa pia kuwaangamiza wapiganaji wa Hamas.
Soma zaidi:Maafisa Gaza wasema watu 19 wameuawa kwenye mashambulizi ya Israel
Wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz alionya juu ya shambulio kali la Israeli iwapo mashambulio ya maroketi kutoka kundi la Hamas yataendelea. Mashambulizi hayo ya maroketi kutokea Gaza yameripotiwa wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kutafuta makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka na usitishaji mapigano yakiwa yameanza tena nchini Qatar.
Wapatanishi wa Qatar, Misri na Marekani wameshirikiana kwa miezi kadhaa katika juhudi za kufikia makubaliano ya kumaliza vita na kuhakikisha kuachiliwa kwa makumi ya mateka lakini hatua hizo hazijazaa matunda.