1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakataa kusitisha mapigano na Hezbollah

26 Septemba 2024

Waziri wa Fedha wa Israel, Israel Bezalel Smotrich, anayeegemea mrengo mkali wa kulia amelipinga na kulikataa kabisa pendekezo la kusitishwa mapigano kati ya Israel na Lebanon kwa siku 21.

https://p.dw.com/p/4l6FK
Waziri wa Fedha wa Israel, Israel Bezalel Smotrich
Waziri wa Fedha wa Israel, Israel Bezalel SmotrichPicha: Bezalel Smotrich/newscom/picture alliance

Smotrich, mjumbe muhimu katika serikali ya mseto ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, amelipinga pendekezo hilo, akisisitiza kwamba kuendeleza vita dhidi ya Hezbollah ndiyo njia pekee inayopaswa kufuatwa na Israel ili kulisambaratisha kundi la Hezbollah.

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa António Guterres aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana kwamba nchi ya Lebanon inatumbukia kuzimu alipobainisha kwamba siku ya Jumatatu ilikuwa ni siku ambayo kizazi cha Lebanon kilishuhudia umwagikaji damu mkubwa.

Marekani | Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa | New York | Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa António GuterresPicha: Richard Drew/AP Photo/picture alliance

Guterres ametoa mwito wa kuendelezwa juhudi za kuumaliza uhasama kati ya Israel na kundi la Hezbollah:

"Ninaliomba baraza hili kufanya kazi bila kuchoka ili kuuzima moto huu. Pande zote ni lazima zikubali mara moja kusitisha uhasama na kuchukua hatua halisi kuelekea utekelezaji kamili wa maazimio 1559, na 1701. Raia lazima walindwe na miundombinu ya kiraia haipaswi kulengwa.”

Marekani, Umoja wa Ulaya na washirika wengine yakiwemo mataifa kadhaa ya Kiarabu walitoa mwito wa pamoja wa kusitisha mapigano kwa siku hizo 21 nchini Lebanon baada ya mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya kundi la Hezbollah kusababisha vifo vya mamia ya watu nchini Lebanon huku maelfu wengine wakilazimika kuyahama makazi yao wiki hii.

Soma Pia: Netanyahu asema hatasikia la mtu huku vita vya Gaza vikiendelea kupamba moto 

Wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa wiki tatu ulitolewa saa chache baada ya mkuu wa jeshi la Israel Luteni Jenerali Herzi Halevi siku ya Jumatano kuwaambia wanajeshi wa Israel wajiandae kwa sababu kuna uwezekano wa Israel kufanya mashambulizi ya ardhini dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hezbollah.

Hii leo Alhamisi, jeshi la Israel limechapisha video inayoonesha mashambulizi yake ya usiku kucha dhidi ya maeneo iliyoyalenga ya Hezbollah. IDF imesema katika taarifa yake kwamba imeshambulia takriban maeneo 75 ya Hezbollah katika eneo la Beqaa na kusini mwa Lebanon.

Israel - Benjamin Netanjahu na Bezalel Smotrich
Mbele Kulia: Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich. Kushoto: Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/Pool Reuters/AP/dpa

Qatar, mpatanishi katika vita vya Gaza, imesema hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na msukumo wa kimataifa wa kusitishwa mara moja kwa mapigano kati ya Hezbollah nchini Lebanon na Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesema vita vya Gaza vitaendelea hadi malengo yote ya Israel katika vita hivyo yatakapotimia.

Vyanzo: AFP/RTRE