Miito yaongezeka ya kuwepo taifa huru la Palestina
22 Januari 2024Israel ambayo imeapa kulitokomeza kundi hilo, imetupilia mbali miito ya uwepo wa taifa huru la Palestina na kusema wataendelea kuwa na udhibiti wa usalama huko Gaza hata baada ya vita hivyo kumalizika.
Mshirika wake mkuu, Marekani na nchi nyingine kadhaa, wamependekeza kwamba suluhisho la mataifa mawili ndio njia pekee ya kuhakikisha usalama wa kudumu wa pande zote.
Kabla ya mkutano na wajumbe wa Israel na Palestina, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesisitiza juu ya suluhisho la mataifa mawili na kusema Israel haiwezi kudumisha amani kwa kwa mtuto wa bunduki. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema uwepo wa mataifa mawili ya Israel na Palestina ndio suluhu pekee katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.
" Israel wataweza kuishi kwa usalama ikiwa tu Wapalestina nao wataishi kwa usalama na kwa heshima. Na Wapalestina wanaweza kuishi kwa heshima, kwa usalama na kwa uhuru ikiwa Israel itaweza kuishi kwa usalama. Ndio maana suluhu la mataifa mawili ndilo suluhu pekee, na wale wote wanaokataa kutambua hilo hadi sasa hawajapendekeza njia mbadala.”
Soma pia: Hamas: Zaidi ya watu 25,000 wameuwawa wakati Israel ikiendeleza mashambulizi yake Gaza
Mawaziri 27 wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watakutana na waziri wa mambo ya nje wa Israel Israel Katz, kabla ya kuzungumza na mwanadiplomasia mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Riyad al-Maliki. Mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Jordan na Saudi Arabia pia watafanya mazungumzo na mawaziri hao wa Ulaya.
Mashambulizi yaendelea huko Gaza
Mapambano makali kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas yameripotiwa usiku wa kuamkia leo katika mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis. Ghasia zimeongezeka pia katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel.
Katika ripoti yake ya kwanza kwa umma, kundi la Hamas lilikiri baadhi ya makosa katika matukio ambayo yalianzisha vita hivyo lakini pia likatoa wito wa kukomeshwa kwa kile walichokiita "uchokozi wa Israel" huko Gaza. Hamas imedai shambulio la Oktoba 7 ilikuwa "hatua muhimu" dhidi ya uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina.
Soma pia: Netanyahu anapinga wazo la kuipa mamlaka ya Palestina udhibiti katika ukanda wa Gaza
Familia za mateka takriban 132 ambao bado wanashikiliwa huko Gaza wamemtaka Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufikia makubaliano na kundi la Hamas ili mateka hao waweze kuachiliwa huru.
Netanyahu amesema Hamas wametoa masharti ya kuachiwa mateka hao ambayo hayakubaliki. Hamas inataka vita visitishwe, kuondolewa kwa vikosi vyote vya Israel huko Gaza, kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina na kuhakikishiwa itasalia madarakani.
(Vyanzo: Mashirika)