Israel yafanya mashambulizi mabaya katika ukanda wa Gaza
23 Mei 2024Israel imefanya mashambulizi mabaya ya anga katika ukanda wa Gaza mapema leo huku ikisema kuwa iko tayari kuanza tena mazungumzo yaliokwama na kundi la wanamgambo la Hamas kuhusu makubaliano na pia kuachiwa huru kwa mateka ili kusitisha vita vinavyoendelea katika eneo hilo tangu Oktoba 7.
Idara ya ulinzi wa raia katika ukanda wa Gaza, imesema mashambulizi mawili ya anga alfajiri ya leo yamesababisha vifo vya watu 26 wakiwemo watoto 15 mjini Gaza City pekee.
Soma pia: Makombora ya anga ya Israel yauwa 35 Gaza
Msemaji wa idara hiyo Mahmud Bassal, amesema shambulizi moja lililenga nyumba moja ya familia na kuwauwa watu 16 katika eneo la Al-Daraj na lingine kuwauwa watu 10 ndani ya kiwanja cha msikiti.
Hakukuwa na tamko la haraka kutoka kwa jeshi la Israel.
Mapigano makali ya barabarani pia yalizuka katika maeneo ya Jabalia na Rafah ambapo makundi yenye silaha ya Hamas na mshirika wake Islamic Jihad yamesema yamewafyatulia risasi wanajeshi wa Israel.