1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Israel yafanya mashambulizi nchini Iran

26 Oktoba 2024

Kituo cha utangazaji cha serikali ya Iran kiliripoti mapema siku ya Jumamosi angalau milipuko sita katika mji mkuu Tehran na karibu na jiji la Karaj. Israel, ilikiri kushambulia vituo vya kijeshi nchini humo.

https://p.dw.com/p/4mFjL
Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiongoza kikao cha Baraza la Usalama baada ya mashambulizi ya makombora ya Iran nchini Israel Oktoba 1, 2024Picha: Avi Ohayon (GPO)/Handout/Anadolu/picture alliance

Hakukua na tamko lolote la mapema kuhusiana na chanzo cha milipuko hiyo, ingawa muda mfupi baadae, Jeshi la Israel, IDF liliarifu kupitia mtandao wa X kwamba limevishambulia vituo vya kijeshi nchini Iran.

Sehemu ya taarifa hiyo ilisema, IDF ilichukua hatua hiyo kujibu mashambulizi ya mfululizo yaliyofanywa na Iran dhidi ya taifa la Israel.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa utawala wa Iran na washirika wake wa kikanda wamekuwa wakiishambulia Israel kwa mfululizo tangu Oktoba 7, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya moja kwa moja kutokea Iran.

"Kama ilivyo kwa taifa lolote huru ulimwenguni, Taifa la Israel lina haki na jukumu la kujibu," iliongeza taarifa hiyo.

Soma pia:Hofu yatanda Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi ya Iran

Iran Tehran
Mji wa Tehran, Iran kama unavyoonekana pichani nyakati za usikuPicha: Arne Bänsch/dpa/picture alliance

Israel imekuwa ikipanga kujibu shambulizi la makombora lililofanywa na Iran Oktoba 1, ambalo lilikuwa ni la pili kufanywa, moja kwa moja kutokea Iran katika kipindi cha miezi sita.

Mamlaka za Iran hapo kabla ziliionya Israel dhidi ya kufanya shambulizi lolote, ikisema hatua kama hiyo dhidi ya Iran itajibiwa vikali.

Ikulu ya White House: Shambulizi la Israel nchini Iran "ni hatua ya kujilinda"

Ikulu ya White House, imesema mashambulizi haya ya Israel nchini Iran "ni hatua ya kujilinda", kufuatia shambulizi la makombora la Iran mwanzoni mwa mwezi huu.

Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa Sean Savett amesema "mashambulizi yaliyolenga vituo vya kijeshi" yalikuwa ni hatua ya kujilinda na ya kujibu shambulizi la makombora dhidi ya Israel, Oktoba 1."

Soma pia:Iran yaishambulia Israel kwa makombora 180