Israel kusitisha mapigano Gaza kupisha chanjo ya Polio
30 Agosti 2024Israel imechukua hatua hiyo ili kuwezesha maafisa wa afya kutoa chanjo ya polio kwa watoto katika Ukanda wa Gaza.
Rik Peeperkorn, mwakilishi wa shirika hilo kwenye maeneo ya Palestina amesema kulingana na makubaliano, kampeni hiyo ya chanjo itaanza Septemba mosi katika eneo lote la Gaza.
Michael Ryan, naibu mkurugenzi mkuu wa WHO, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu umuhimu kwa pande zote kuzingatia ahadi hizo ambazo zimetolewa.
Soma pia: Wito wa vita kusitishwa Gaza kupisha chanjo ya polio
Kampeni hiyo inalenga kutoa chanjo ya Polio kwa zaidi ya watoto 640,000 wa Gaza walio chini ya umri wa miaka 10. Virusi vya polio huenea kupitia maji yaliyochafuliwa na vinaweza kusababisha ulemavu na kupooza mwili, na hata kifo.
Hali yazidi kuwa mbaya Gaza
Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza ambako bado kunaripotiwa mapigano makali kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas.
Wakati akielezea mateso ya wakaazi wa Gaza, Afisa wa Umoja wa Mataifa aliliambia Baraza la Usalama siku ya Alhamisi na kuhoji: "nini kimetokea kwa ubinadamu wetu? Ni vigumu kuelezea kwa maneno madhila makubwa ya watu wa Gaza na shida wanazopitia ili kupata makazi au mahitaji mengine ya msingi."
Soma pia: UN yaomba mapigano yasitishwe kuruhusu chanjo kwa watoto Gaza
Kauli hiyo ilitolewa na Joyce Msuya, kaimu mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA), wakati wa mkutano kuhusu hali ya kibinadamu katika eneo lililozingirwa la Palestina.
Bi Msuya amesema wakazi wa Gaza wana njaa, wana kiu, hawana makazi, ni wagonjwa na madhila yao yamepindukia mateso ambayo mwanadamu yeyote anaweza kuvumilia. Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya vifo sasa imefikia watu 40,602.
(Vyanzo: AP, DPAE, AFP)