1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Wamarekani watano wawekwa chini ya kifungo cha nyumbani Iran

11 Agosti 2023

Raia watano wa Marekani wanaozuiliwa nchini Iran wameachiliwa kutoka jela moja nchini humo na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani. Mvutano kati ya mataifa hayo mawili umekuwa ukiongezeka katika siku za hivi karibuni

https://p.dw.com/p/4V2da
Picha hii isiyo na tarehe iliyotolewa na Babak Namazi, ambaye ni kaka ya Siamak Namazi na mwana wa Baquer Namazi. Picha hii inamuonesha  Baquer Namazi, kushoto, na mwanawe Siamak katika eneo lisilojulikana.
Baquer Namazi ( kushoto) na mwanawe Siamak Namazi (Kulia)Picha: Babak Namazi/AP Photo/picture alliance

Hatua hiyo kwa wafungwa ambao mmoja wao amezuiliwa kwa takriban miaka minane inakuja baada ya diplomasia tulivu na ya kuchosha kati ya mataifa hayo mawili ambayo ni mahasimu wa mda mrefu ambayo mazungumzo yao ya kando kuhusu mkataba wa nyuklia yalivunjika. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, amewaambia wanahabari kuwa imani yake ni kwamba huo ni mwanzo wa kumalizika kwa kizungumkuti kinachowakabili wafungwa hao pamoja na familia zao.

Iran yataja makubaliano hayo kuwa ubadilishanaji wa wafungwa

Iran imeelezea makubaliano hayo kuwa ubadilishanaji wa wafungwa, huku shirika la habari la serikali IRNA likinukuu ujumbe wa nchi hiyo kwa Umoja wa Mataifa ukisema kuwa kila nchi itatoa msamaha na kuwaachilia wafungwa watano. Raia wote watano wa Marekani katika makubaliano hayo wana asili ya Iran. Iran haitambui uraia wa nchi mbili na imekuwa na uhusiano wa kiuhasama na Marekani tangu mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 yaliyoung'oa madarakani utawala wa kifalme wa shah nchini humo uliounga mkono mataifa ya Magharibi.

Wafungwa wanaohusika katika makubaliano hayo

Namazi, mfanyabiashara, alikamatwa mnamo Oktoba mwaka 2015. Alishtakiwa kwa upelelezi katika kile ambacho familia yake imekitaja kuwa ushahidi wa kuchekesha. Babake ambaye alihudumu kama afisa wa UNICEF, Baquer Namazi, alikamatwa alipokwenda kumsaidia mwanawe lakini hatimaye aliruhusiwa kutoka jela mwaka jana kwasababu ya kuzorota kwa afya yake.

Tahbaz, aliyechangia katika uhifadhi wa wanyamapori nchini Iran, alikamatwa pamoja na wanamazingira wenzake mnamo Januari 2018 na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa madai ya kula njama na Marekani. Tahbaz anauraia wa mataifa matatu ambapo pia ni raia wa Uingereza. Aliachiliwa baada ya muda mfupi wa kifungo cha nyumbani mwaka jana wakati wa makubaliano na Uingereza ambayo yalisababisha kuachiliwa huru wa raia wengine wawili wa Uingereza akiwemo mfanyakazi mmoja wa shirika la msaada, Nazanin Zaghari-Ratcliffe.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Mexico Alicia Barcena katika wizara ya mambo ya nje mjini Washington, Alhamisi, Agosti 10, 2023
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Cliff Owen/AP Photo/picture alliance

Sharqi, mwekezaji anayetoa mtaji wa biashara mpya pia alihukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa mashtaka ya upelelezi.

Chanzo kimoja kilichozungumza kwa sharti la kutotambulishwa, kimesema kuwa iwapo mambo yote yatakwenda kama ilivyopangwa, wafungwa hao wa Marekani wanaweza kuondoka nchini Iran mwezi Septemba .

Tayari wafungwa hao wamehamishwa kutoka gereza la Evin mjini Tehran

Wafungwa wanne Siamak Namazi, Emad Sharqi, Morad Tahbaz na mwengine ambaye hakutaka kutambulishwa walihamishwa kutoka gereza maarufu la Evin mjini Tehranla siku moja baada ya utawala wa rais Joe Biden kuziarifu familia zao kuhusu mkataba huo. Wakili wa mmoja wa wafungwa hao amesema kuwa wanne hao walisindikizwa hadi katika hoteli moja na watakuwa chini ya ulinzi. Vyanzo vinaarifu kuwa mfungwa wa tano ambaye ni mwanamke pia ni sehemu ya mazungumzo hayo na tayari amehamishiwa kifungo cha nyumbani katika wiki za hivi karibuni.

Sehemu ya mazungumzo hayo ni kuachiliwa kwa fedha za Iran

Suala kuu katika mazungumzo hayo ni kuachiliwa kwa dola bilioni 6 ambazo Iran ilijipatia baada ya kuiuzia mafuta Korea Kusini. Korea Kusini ilifunga akaunti za Iran kwa kuzingatia vikwazo vya Marekani vilivyowekwa chini ya uongozi wa rais wa zamani wa nchini hiyo, Donald Trump. Hatua hiyo ilivuruga pakubwa uchumi wa Iran.

Vikisisitiza kuwa mpangilio huo sio wa mwisho, vyanzo vinasema kuwa fedha hizo zitabadilishwa kutoka sarafu ya won hadi Euro na kusimamiwa na Qatar ambayo ilitekeleza jukumu kuu la upatanishi. Hakuna fedha zitakazohamishwa moja kwa moja kwa Iran.

Blinken aliweka wazi kwamba fedha hizo tayari ni za Iran na kwamba nchi hiyo haitapokea msamaha wowote wa vikwazo. Blinken pia amesema, "Fedha za Iran zitatumika na kuhamishiwa kwenye akaunti maalumu zitakazothibitiwa ili kwamba zitumike tu kwa sababu za kibinadamu. Shirika la habari la serikali ya Iran, limeripoti kuwa wafungwa hao wataachiwa huru pindi pesa hizo zitakapotolewa.