1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakamata meli ya kigeni iliyobeba mafuta 'ya magendo'

28 Januari 2024

Jeshi la walinzi wa mapinduzi wa Iran limeikamata meli ya kigeni iliyokuwa imebeba karibu lita milioni mbili za "mafuta ya magendo" ya dizeli karibu na Pwani ya kusini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4bleV
Picha ya video inaonyesha meli ya mafuta yenye bendera ya Panama iliyokamtwa na jeshi la walinzi wa mapinduzi wa Iran.Picha: Planet Labs PBC/AP/picture alliance

Shirika la habari la Tasnim la Iran limeripoti kuwa meli hiyo "ilikamatwa kwa mujibu wa amri ya mahakama," likimnukuu kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Haidar Honaryan.

Soma pia: Iran yaikamata meli ya mafuta katika Ghuba ya Oman

Honaryan amesema wafanyakazi kumi na wanne wa meli hiyo pia walikamatwa, na kuongeza kwamba walikuwa raia wa "nchi mbili za Asia", bila  ya kuzitaja kwa majina.

Iran, mzalishaji mkuu wa mafuta, ni miongoni mwa mataifa yenye bei nafuu zaidi ya mafuta ya petroli duniani, jambo linalochangia vitendo vya usafirishaji haramu wa mafuta.

Mwezi Septemba, Iran ilikamata meli mbili za mafuta zilizokuwa zikipeperusha bendera za Panama na Tanzania na kuwakamata wafanyakazi wao kwa madai ya kusafirisha mafuta ya magendo katika eneo la Ghuba.