Meli ya Mafuta ya Iran yaelekea Ugiriki kutoka Gibralter
19 Agosti 2019Meli hiyo iliyobadilishwa jina hivi sasa na kuitwa Adria Darya nambari moja badala ya Greece nambari moja imeng'owa nanga Gibralter saa tano za usiku jana. Ratiba ya safari inaonyesha meli hiyo inaelekea Kalamata nchini Ugiriki . Inatarajiwa kuwasili huko jumaapili inayokuja. Balozi wa Iran nchini Uingereza Hamid Baeidinejad amethibitisha kupitia mtandao wa instagram mapema kwamba meli hiyo "imeshaondoka Gibralter baada ya kuzuwiliwa kwa siku 45."
Gibralter yaruhusu meli ya mafuta ya Iran ing'owe nanga
Meli ya mafuta ya Iran ilikamatwa na jeshi la wanamaji la Uingereza julai 4 iliyopita kwa tuhuma za kusafirisha mafuta hadi Syria kinyume na vikwazo vya Umoja wa ulaya. Kisa hicho kilizusha mvutano uliodumu wiki kadhaa kati ya Teheran na nchi za magharibi. Kimezidisha makali pia ya mvutano katika njia za kimataifa za kusafirishia mafuta katika Ghuba.
Gibralter, eneo linalodhibitiwa na Uingereza ilibatilisha amri ya kuzuwiliwa meli hiyo alkhamisi iliyopita lakini siku ya pili yake korti kuu ya mjini Washington ikachapisha waranti kutaka meli hiyo izuwiliwe. Maafisa wa Gibralter wamesema hawawezi kutekeleza matakwa hayo kwasababu wanalazimika kufuata asheria za Umoja wa ulaya.Washington inataka meli hiyo izuwiliwe kwa hoja za kuwepo mafungamano pamoja na tume ya walinzi wa mapinduzi ya kiislam ambayo Marekani inawataja kuwa magaidi.
Iran inaonya dhidi ya meli yake kuzuwiliwa tena na Marekani
Viongozi wa Ugiriki hawakusema chochote kuhusiana na mvutano huo. Akiulizwa kama Marekani inaweza kutoa tena maombi ili meli hiyo ikamatwe, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Iran. Abbas Mousavi amesema tunanukuu:"Hatua kama hiyo na pia mjadala kuhusu suala hilo yatahatarisha usalama wa safari za meli baharini. Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Musavi amesema Iran imetuma onyo kupitia njia rasmi na hasa kwa ubalozi wa Uswisi, na maafisa wa Marekani wasifanye makosa kama hayo kwasababau anasema "matokeo yake yatakuwa mabaya."
Itafaa kusemam hapa kwamba Uswisi ndiyo inayowakilisha masilahi ya Marekani nchini Iran.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef