1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Iran yaipa onya kali Israel isijaribu kujibu mashambulizi

16 Aprili 2024

Iran imeikumbusha Israel kwamba ikichukuwa hatua ya kuishambulia tena, Tehran itakuwa tayari kujibu mapigo ndani ya muda wa sekunde chache. Jumuiya ya kimataifa nayo imeendeleza kutowa kauli za kuiunga mkono Israel.

https://p.dw.com/p/4erAJ
Iran Teheran | Migogoro |  Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei akizungumza wakati wa mkutano na wanasiasa, maafisa wa serikali ya Iran na maafisa wa kijeshi mjini Tehran.Picha: Iranien Supreme Leader/ZUMA Wire/IMAGO

Ndani ya  Israel kwenyewe, ripoti zinasema baraza la mawaziri lenye jukumu la kusimamia vita linajiandaa kukutana kwa mara ya tatu leo katika kipindi cha siku tatu, katika kikao ambacho kinalenga kutowa maamuzi kuhusu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Iran.

Ni kikao ambacho kinafanyika wakati jumuiya ya kimataifa inaishinikiza Israel kujiepusha kuutanuwa mgogoro katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.

Mkuu wa majeshi wa Israel Herzi Halevi alishatowa ahadi tangu Jumamosi kwamba nchi hiyo lazima itachukuwa hatua kujibu mashambulizi ya zaidi ya makombora 300, droni na maroketi yaliyofyetuliwa na Iran dhidi ya nchi hiyo, japo hakutowa ufafanuzi wa kitakachofanyika.Soma pia: Ukanda wa Gaza waendelea kushambuliwa na Israel

Pamoja na hayo Jumuiya ya Kimataifa kuanzia Washington hadi Brussels, kauli zinazotolewa na viongozi zinaonesha kuiunga mkono Israel huku pia ikiiomba ijiepushe na vita vipana zaidi.

Soma pia:Israel kupunguza operesheni zake za kijeshi Gaza, huku idadi ya waliokufa ikizidi 24,000

Rais Joe Biden wa Marekani alimwambia waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kwamba Marekani pamoja na kuwa mshirika wake haitoshiriki katika mashambulizi ya ulipizaji kisasi.

Hii leo Jumanne Marekani na washirika wake wa Umoja wa Ulaya kwa pamoja wameshikana katika hatua ya kutangaza vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Iran, kama hatua ya kuishawishi Israel kujiepusha kulipa kisasi.

Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen ametahadharisha kwamba wako tayari kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya Iran..Soma pia: Mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel yalaaniwa kimataifa

Ujerumani yakumbusha vikwazo dhidi ya droni za Iran

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ambaye baadaye leo anaelekea Tel Aviv ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kupitisha vikwazo vipya dhidi ya mifumo ya teknolojia ya uundaji droni ya Iran, akikumbusha kwamba umoja huo ulikubaliana mwaka jana kupitisha vikwazo hivyo na kwa hivyo sasa ndio wakati sahihi.

Ujerumani | Diplomasia | Waziri wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.Picha: Florian Gaertner/AA/picture alliance

"Niliendesha kampeni mwishoni mwa msimu wa mapukutiko pamoja na Ufaransa na washirika wengine ndani ya Umoja wa Ulaya, kuhakikisha vikwazo hivi kuhusu mifumo ya uundaji droni vinaendelezwa dhidi ya Iran na washirika wake katika Mashariki ya Kati." Alisema Baerbock

Aliongeza kwamba "vikwazo hivyo viwekwe pia dhidi ya teknolojia nyinginezo za utengenezaji makombora ndani ya Iran. Na natumai kwamba sasa tunaweza hatimae kuchukuwa hatua kwa pamoja kama Umoja wa Ulaya.''

Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 27 uliiwekea vikwazo chungunzima Iran katika miaka ya hivi karibuni kutokana na harakati zake ikiwemo za kuipelekea Urusi droni.

Soma pia:Scholz, Biden waonya juu ya kutoidhinishwa msaada kwa ajili ya vita vya ukraine

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock anakuwa mwanadiplomasia wa kwanza wa ngazi za juu kuitembelea Israel tangu iliposhambuliwa na Iran, na lengo la ziara yake ni kwenda kuihakikishia nchi hiyo mshikamano wa Ujerumani.

Lakini pia ataitumia ziara yake Tel Aviv kushinikiza msaada zaidi wa kiutu uruhusiwe kuingia Gaza.

Wakati huo huo, kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametowa mwito wa kufanyika juhudi mpya za mataifa yote yenye ushawishi kuidhibiti hali mbaya inayoshuhudiwa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ambako inaelezwa raia wanakabiliwa na janga kubwa ambalo linapaswa kushughulikiwa haraka.

Msemaji wa Turk akifafanuwa kuhusu mazingira yanayojitokeza Ukingo wa Magharibi amesema vurugu katika eneo hilo ni suala linaloibuwa wasiwasi mkubwa sana.

Israel inatuhumiwa kuendelea kuzuia uingizaji na usambazaji misaada Ukanda wa Gaza na kukiuka sheria ya kimataifa.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW