Iran na Saudi Arabia zarejesha mahusiano ya kidiplomasia
6 Aprili 2023Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na mwenzake wa Saudia Mwanamfalme Faisal bin Farhan, pande hizo mbili ziliapa kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuboresha uhusiano.
Taarifa ya pamoja imesema pande hizo mbili zilisisitiza umuhimu wa kufuatilia utekelezaji wa Mkataba wa Beijing na uanzishaji wake kwa njia ambayo itapanua uaminifu wa pande zote. Katika kanda fupi iliyorushwa na kituo cha televisheni serikali ya China CCTV, viongozi hao wa Saudi Arabia na Iran walionekana wakisalimiana kwa bashasha.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang ndiye alieshuhudia kusainiwa kwa taarifa hiyo ya pamoja kati ya Saudi Arabia na Iran.
''Hatua muhimu kusaka amani Mashariki ya Kati''
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen pia walikuwa katika mji mkuu wa China Alhamisi. Macron alikaribisha hatua ya Iran na Saudia huku akimpongeza mwenzake wa China kwa kufikia hatua muhimu.
''Kuhusiana na hali ya Mashariki ya Kati, China ilianzisha maelewano kati ya Saudi Arabia na Iran na ni nawapongeza kuhusu maendeleo haya muhimu sana.", alisema Macron.
Mkutano huo umekuja baada ya makubaliano ya mshangao yaliyofikiwa na Tehran na Riyadh chini ya upatanishi wa China mwezi Machi, ili kurejesha uhusiano ambao ulikuwa umekatika miaka saba iliyopita wakati waandamanaji nchini Iran waliposhambulia ofisi za kidiplomasia za Saudia.
Maafisa kutoka Iran na Saudi Arabia walifanya duru kadhaa za mazungumzo huko Baghdad na Oman kabla ya kukutana mjini Beijing. Mazungumzo kati ya mawaziri hao wa mambo ya nje yanatarajiwa kufuatiwa na ziara ya rais wa Iran Ebrahim Raisi mjini Riyadh. Serikali ya Iran imesema rais Ebrahim Raisi alikubali mwaliko kutoka kwa Mfalme Salman wa Saudi Arabia.
Nchi hizo zimesema katika taarifa ya pamoja kwamba zitazindua mipango ya kufungua tena balozi na balozi ndogo kwenye nchi zao ndani ya kipindi cha miezi miwili kilichoainishwa katika makubaliano ya mwezi uliopita.
Mafanikio ya China katika kuzileta pamoja Iran na Saudi Arabia ni changamoto kubwa kwa Marekani ambayo kwa muda mrefu iliongoza sera za nje za Mashariki ya Kati.