India yashika namba mbili kuwa na visa vingi vya COVID-19
7 Septemba 2020Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, katika kipindi cha saa 24, India imerekodi visa vipya 90,802 na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa na visa milioni 4.2 ikiwa nyuma ya Marekani yenye visa milioni 6.2.
Siku ya Jumatatu Wizara ya Afya ya India pia imerekodi vifo vipya 1,016 na kufanya jumla ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 kufikia 71,642, ikiwa nchi ya tatu duniani yenye vifo vingi.
Katika wiki za hivi karibuni, India ambayo ni ya pili duniani kwa kuwa na watu wengi wanaofikia bilioni 1.4, imekuwa eneo jipya lenye visa vingi vya virusi vya corona, ingawa visa vinaendelea kuongezeka ulimwenguni kote ambako kuna wagonjwa takriban milioni 27 na zaidi ya vifo 880,000.
Ufaransa, Israel na Australia ni miongoni mwa nchi zilizolazimika katika siku za hivi karibuni kuongeza vizuizi vya usafiri au kuweka vingine vipya katika juhudi za kudhibiti maambukizi mapya.
Vituo vya treni vyafunguliwa
Hata hivyo, India Jumatatu imekifungua tena kituo cha treni kwenye mji mkuu, New Delhi ambacho kilifungwa kwa takriban miezi sita na kwenye miji mingine 12 vituo vya treni za chini ya ardhi pia vimefunguliwa tena. Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Reli la New Delhi, A. K. Gang amesema safari hizo zitazingatia suala zime la usafi.
''Tumeandaa mipango yote ili kuhakikisha usafiri unakuwa salama kabisa na ni uamuzi sahihi kwamba huduma za treni zimeanza. Watu walikuwa wanasubiri usafiri wa treni kuanza, kwa sababu Delhi leo inategemea usafiri wa treni,'' alifafanua Gang.
Nchini Uhispania serikali inajaribu kuzifungua tena shule, ingawa nchi hiyo imerekodi idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya virusi vya corona barani Ulaya.
Naye waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi anaendelea vizuri na matibabu ya maradhi ya COVID-19. Daktari wake Alberto Zangrillo, amewaambia waandishi habari kuwa Berlusconi, mwenye umri wa miaka 83 aliyelazwa wiki iliyopita kutokana na matatizo ya mapafu, anaendelea vizuri na tiba.
Huko nchini Uingereza, Waziri wa Afya, Matt Hancock amesema ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini humo linatia wasiwasi, ingawa amefafanua kwamba serikali bado inalidhibiti janga hilo. Jana Uingereza ilirekodi visa vipya 2,988, idadi ya juu kurekodiwa tangu mwezi Mei.
Naye kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi siku ya Jumatatu aliondoka kwenye shughuli yake ya kwanza ya kampeni, kutokana na mripuko wa virusi vya corona nchini humo. Jumapili Myanmar iliripoti visa vipya 100 vya maambukizi ya virusi hivyo, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kwa siku kuwahi kuripotiwa tangu kisa cha kwanza cha maambukizi nchini humo kitangazwe mwezi Machi.
(AFP, DPA, AP, Reuters)