India, Canada zafukuziana mabalozi katikati mwa mzozo mkubwa
14 Oktoba 2024India na Canada kila moja ilimfukuza balozi wa nchi nyingine pamoja na wanadiplomasia wengine watano, kufuatia madai ya New Delhi kwamba balozi wake ametajwa kati ya "watu wanaoshukiwa" kuhusiana na mauaji ya kiongozi wa wanaharakati wa kujitenga wa Masingasinga.
Mgogoro wa kidiplomasia uliibuka baada ya New Delhi kusema kuwa inawaondoa wanadiplomasia wake sita kutoka Canada, huku Ottawa ikitangaza kuwa imewatolea hati za kufukuzwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Melanie Joly, alisema India ilikataa kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa mauaji ya Hardeep Singh Nijjar, raia wa Canada aliyeuawa mwaka 2023, na haikuondoa kinga ya kidiplomasia kwa wanadiplomasia wake.
Soma pia: Canada yawaondoa wanadiplomasia 41 kutoka India
Alisisitiza kuwa uamuzi wa kuwafukuza watu hao ulifanywa baada ya Polisi ya Kifalme ya Canada (RCMP) kukusanya ushahidi wa kutosha unaowahusisha na uchunguzi.
Kuzorota kwa Mahusiano ya Kidiplomasia
Mgogoro ulizidi kuwa mkubwa baada ya India kumfukuza Kaimu Balozi wa Canada, Stewart Wheeler, naibu wake, na makatibu wanne wa kwanza. Ottawa ilijibu kwa njia sawa, huku polisi wa Canada wakitoa ushahidi unaounganisha mawakala wa serikali ya India na shughuli za uhalifu mkubwa.
Mauaji ya Nijjar, ambaye alikuwa mtetezi wa kuundwa kwa taifa huru la Masingasinga, Khalistan, yalizua mgawanyiko mkubwa katika mahusiano ya India na Canada baada ya Waziri Mkuu Justin Trudeau kuishutumu idara ya kijasusi ya India kuhusika na uhalifu huo.
India imekana tuhuma hizo, ikiziita "zisizo na msingi" na ikailaumu serikali ya Trudeau kwa kuunga mkono misimamo mikali na ya kujitenga dhidi ya India.
Licha ya mgogoro huo, kila nchi inaendelea kushikilia misimamo yake, huku India ikitishia kuchukua hatua zaidi na Canada ikisisitiza kushirikiana ili kutatua tuhuma hizo.
Mzozo waongeza shinikizo kwa Trudeau
Canada ni nyumbani kwa karibu Masingasinga 770,000, ambao wanaunda takriban asilimia mbili ya wakazi wa nchi hiyo, huku watu wachache wakitoa wito wa kuundwa kwa taifa huru la Khalistan.
Mnamo Novemba 2023, Wizara ya Sheria ya Marekani pia ilimshtaki raia wa India anayeishi Jamhuri ya Czech kwa madai ya kupanga jaribio kama hilo la mauaji katika ardhi ya Marekani.
Soma pia: Justin Trudeau amuangusha Stephen Harper Kanada
Waendesha mashtaka walisema katika hati za mahakama ambazo hazijafunguliwa kwamba afisa wa serikali ya India pia alihusika katika kupanga jaribio hilo.
Mzozo huo unajiri wakati Trudeau akiwa chini ya shinikizo la kisiasa nyumbani, baada ya kunusurika katika kura ya pili ya kutokuwa na imani naye mapema mwezi huu.