Justin Trudeau amuangusha Stephen Harper Kanada
20 Oktoba 2015Kwa Wakanada wengi uchaguzi huu ulikuwa kura ya maoni kuhusu mfumo wa utawala wa Harper, aliekosolewa kuwa mkandamizaji na pia juu ya nani yuko katika nafasi nzuri zaidi ya kurekebisha uchumi wa taifa hilo unaoyumba.
Trudeau mwenye umri wa miaka 43, aliahidi kupandisha kodi kwa matajiri na kuzishusha kwa watu wa tabaka la kati. Mwana huyo wa kwanza wa waziri mkuu wa zamani maarufu Pierre Trudeau, alieendesha kampeni ya ushindani kwa kile alichokiita maono mapya kwa ajili ya taifa hilo, ameshinda zaidi ya viti 188 kati ya jumla ya viti 338 vya ubunge.
Chama chake kilichomoza kutoka nafasi ya tatu hadi usoni mwishoni wa kampeni, ambapo Trudeau, mtoto wa kwanza wa Pierre Trudeau - anaechukuliwa kuwa mwasisi wa Canada ya sasa -- aliahidi "siyo tu mabadiliko ya serikali, bali pia serikali bora."
'Shetani wa Trudeau'
"Wakanada wamenena, mnataka serikali yenye maono na ajenda chanya, yenye kiu ya kusonga mbele na ya matumaini kwa nchi hii. Nawahidi leo marafiki zangu, kwamba nitaiongoza serikali hiyo," alisema Trudeau katika hotuba yake ya ushindi, na kuahidi kuyafanya aono hayo kuwa halisi. "Nitakuwa waziri mkuu huyo."
Trudeau alichaguliwa kukiongoza chama cha Kiliberali miaka miwili tu iliyopita, baada ya viongozi wawili wa zamani kushindwa kumuondoa Harper mwaka 2008 na 2011 na hatimaye kujiuzulu.
Anaonakana kufanikisha ndoto yake ya kurejesha kile kinachofahamika kama "Shetani wa Trudeau", yaliyompeleka baba yake maradakani mwaka 1968. "Bila shaka kulikuwepo aina fulani ya "Shetani mdogo wa Trudeau" katika kampeni," alisema Claude Denis, profesa wa siasa katika chuo kikuu cha Ottawa.
Harper akubali kushindwa
Stephen Harper alieingia madarakani mwaka 2006 na alikuwa akiwania muhula wa nne, alikubali kushindwa na chama chake kikatangaza amejiuzulu wadhifa wake wa kiongozi mkuu wa chama. Katika hotuba yake ya kukubali kushindwa Harper alisema watu kamwe hawafanyi makosa.
"Nchi yetu ni moja ya demokrasia imara zaidi duniani kwa sasa. Na hii leo kwa mara ya 42 katika kipindi cha miaka 148 Wacanada wamechaguwa bunge la taifa. Wakati matokeo haya siyo tuliyoyatarajia, tunaamini kuwa watu hawakosei kamwe,alisema Harper.
Kampeni ndefu zaidi katika historia
Kampeni za uchaguzi huu zilizodumu kwa wiki 11 ndizo zilikuwa ndefu zaidi katika historia ya Kanada na ziliwapa fursa wapiga kura kuwafahamu vizuri viongozi wa vyama na mawazo yao katika mijadala mitano na karibu hotuba za kila siku.
Mbali na ahadi ya kupandisha kodi kwa matajiri zaidi na viwango vya chini kwa Wacanada wa kipato cha kati, Trudeau alisema atatumia mabilioni kwenye maendeleo ya miundombinu na kuuimarisha uchumi wa taifa hilo unaochechemea. Pia aliahidi kuhalilisha matumizi ya marijuana.
Masuala makuu ya kampeni
Miongoni mwa masuala yaliyoghubika mijadala ya wagombea ni kuhusu namna Canada inavyopasa kushughulikia wakimbizi wanaotoroka vita nchini Syria, hukumu ya mahakama iliyobatilisha marufuku dhidi ya vazi la kufunika uso - Niqab, na mdororo wa kiuchumi.
Chama cha kinachoegemea mrengo wa kushoto cha New Demcracy, kinachoongozwa na Thomas Mucair, kilitaraji kujiimarisha kutoka nafasi yake ya pili kiliyopata katika uchaguzi wa 2011, na kuongoza kwa mara ya kwanza. Lakini badala yake kimemaliza kikiwa katika nafasi ya tatu.
"Uchaguzi huu ulihusu zaidi mabadiliko na usiku huu Wakanada wamefunga ukurasa wa miaka 10 ya utawala wa Harper," alisema Mulcair katika hotuba yake ya kukubali kushindwa.
Mhemko wa kampeni
Wakati mwingine mapambano yalipelekea mashambulizi dhidi ya haiba ya mtu, ambapo matangazo ya kampeni ya wahafidhina yalikuwa yakiashiria kuwa Trudeau, na muonekano wake mzuri wa kijana -- hakuwa tayari kuwa waziri mkuu.
Lakini mpambano huo mrefu ulimpa nafasi ya kuimarisha mbinu zake za kampeni, na kuwapa Wakanada fursa ya kumfahamu vizuri. Maisha yake ya zamani yanahusisha kazi yake kama mkufunzi wa skii ya ubao, mhudumu wa baa na mzuwia fujo. Kufikia siku ya uchaguzi, Trudeau alikuwa amepoteza sauti yake.
Wachambuzi wa siasa tayari wameanza kukisia juu ya muundo wa serikali ya Trudeau, huku wakitafakari kuhusu kilichosababisha anguko la Harper, mwenye umri wa miaka 56, ambaye amekosolewa kwa kujiweka mbali na raia, lakini akimuagiwa sifa kwa kusimamia uchumi katika muongo uliogubikwa na mashaka katika sekta ya fedha.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Caro Robi