UN: Kaya zilitupa milo bilioni 1, mwaka 2022.
27 Machi 2024Zaidi ya chakula chenye thamani ya dola trilioni 1 kilitupwa kutoka kwenye kaya na wafanyabiashara wakati ambapo karibu watu milioni 800 walikuwa wakikabiliwa na njaa, hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya hivi karibuni zaidi ya Umoja wa Mataifa ya Fahirisi ya Taka za Chakula.
Ripoti hiyo imesema zaidi ya tani bilioni 1 za chakula -- karibu moja ya tano ya mazao yote yanayopatikana sokoni -- kiliharibiwa mwaka 2022, na kiwango kikubwa kikimwagwa na kaya mbalimbali.
Soma pia:UN: Watu milioni 5 wakabiliwa na baa la njaa Sudan
"Upotevu wa chakula ni janga la kimataifa. Mamilioni ya watu watakuwa na njaa leo kama chakula kinaharibiwa kote ulimwenguni," Inger Andersen, mkurugenzi mtendaji wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, UNEP, alisema.
Uchafu utokanao na chakula huzalisha joto mara tano zaidi ya sekta ya anga. Ripoti hiyo, iliyoandikwa na shirika lisilo la faida la WRAP, ni ya pili tu inayohusiana na upotevu wa chakula duniani na iliandaliwa na Umoja wa Mataifa na ambayo inatoa uihalisia zaidi hadi sasa.
Soma pia:UN: Dunia hatarini kutokana na mawimbi ya joto
Ripoti hiyo hata hivyo imesema takwimu hizo zinaweza kuwa kubwa kuliko makadiro yaliyotolewa.
"Kwangu mimi, inashangaza," Richard Swannell kutoka WRAP aliiambia AFP. "Unaweza kuwalisha watu wote ambao kwa sasa wana njaa duniani -- takriban watu milioni 800 -- kwa siku kutokana na chakula kinachotupwa kila mwaka."
Amesema hatua ya kuwakutanisha pamoja wazalishaji na wauzaji wa rejareja imesaidia kupunguza uharibifu na kupata chakula kwa ajili ya wenye mahitaji, na hilo linahitajika kufanyika zaidi.
Asilimia 28 ya chakula ilitupwa kutoka kwenye maeneo ya kuuza vyakula kama migahawa, kantini na hoteli na kwenye maeneo kama ya wachinjaji na biashara za rejareja kama vile wauzaji mboga mboga wakimwaga vyakula kwa asilimia 12.
Lakini kiasi kikubwa cha chakula kilimwagwa kutoka kwenye kaya zilizochangia asilimia 60 -- kama tani milioni 631.
Swannell alisema hii ilisababishwa na kaya nyingi kununua chakula kingi kuliko walichokihitaji na kutokula vyakula vilivyobaki ama viporo na vyakula vingine kufikia muda wa mwisho wa matumizi.
Chakula kingi, haswa katika matafa masikini, hakikutupwa kiholela, lakini badala yake kilipotea wakati kinasafirishwa ama kuharibika kwa sababu ya kukosa majokofu, ilisema ripoti hiyo.
Swannel amesema kama taka za vyakula ingekuwa ni nchi, basi ingekuwa ni ya tatu kwa uzalishaji wa gesi chafu ulimwenguni, ikitanguliwa na Marekani na China.
Lakini watu hawafikirii hilo, "licha ya kwamba ingeweza kusaidia si tu katika kupunguza uzalishaji huo wa hewa chafu bali pia kuokoa fedha kwa kuwa na matumizi mazuri ya chakula wanachokinunua," amesema Swannel.