IMF yaonya juu ya ruzuku za mabadiliko ya tabia nchi
20 Januari 2023Akizungumza katika Kongamano la kimataifa kuhusu uchumi mjini Davos Uswisi, Georgieva ameelezea wasiwasi kwamba suala la kuhimiza mabadiliko ya uchumi wa kijani kwa kutumia fedha za umma ili kuongeza uwekezaji binafsi, linaweza lisiwe na mantiki kwa uchumi unaochipukia. Ametahadharisha kuwa ruzuku hizo zinaweza kuchochea teknolojia na uzalishaji wa nchi maskini kuhamishiwa kwa nchi tajiri.Teknolojia rafiki yajadiliwa katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia
Marekani chini ya rais Joe Biden imepitisha sheria ya kupunguza mfumuko wa bei ijulikanayo kama IRA, ambayo inajumuisha ruzuku kubwa na ukataji kodi wenye thamani ya Dola bilioni 370 kwa ajili ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. Mpango huo ni mkubwa kuwahi kuidhinishwa na Marekani wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Umoja wa Ulaya unakusudia pia kukabiliana na hilo katikati mwa wasiwasi kwamba sheria hiyo mpya ya Marekani itawasukuma wafanyabiashara kuhamishia viwanda vyao na uzalishaji Marekani katika wakati ambao muungano huo unapojaribu kuimarisha sekta yake ya viwanda.
Akizungumza kando ya Georgieva, waziri wa uchumi wa Ufaransa Bruno Le Maire ametetea msimamo wa serikali yake wa kuunga mkono juhudi za kuachana na matumizi ya nishati ya ardhini.
Georgieva pia amelieleza kongamano hilo kwamba hali ya kiuchumi kwa mwaka huu inaonekana kuwa sawa kuliko ilivyohofiwa hapo awali, ingawa bado kuna vitisho kama kuongezeka kwa mzozo nchini Ukraine na kuibuka upya kwa vita vya kibiashara.
"Sasa baada ya China kufunguliwa tena, tunatarajia ukuaji wa uchumi mwaka huu kupindukia wastani wa kimataifa. Tunatazamia asilimia 2.7 kwa ulimwengu, hii inaweza kusahihishwa katika siku chache. Kwa upande wa China tunatabiri asilimia 4.4."
Katika hatua nyingine wanaharakati vijana takribani 30 wa mazingira akiwemo Greta Thunberg wameandamana nje ya kongamano la kiuchumi la Davos, wakiwatuhumu viongozi wa ulimwengu kwa kushindwa kuilinda sayari. Wanaharakati hao hawakujali baridi kali kwenye barabara ya kuelekea kongamano la WEF na kubeba mabango yaliyo na ujumbe tofauti sambamba na kupaza sauti za "nini tunakitaka? ni haki kwa mazingira? Lini tunataka? Ni sasa."
Thunberg, ambaye alizuiliwa kwa muda na polisi wa Ujerumani mapema wiki hii wakati wa maandamano dhidi ya upanuzi wa matumizi ya makaa ya mawe, hakuzungumza wakati wa maandamano ya Davos. Thunberg alishiriki katika mjadala kando ya mkutano huo wa WEF siku ya Alhamis na kuwatuhumu wanasiasa wa ulimwengu na wafanyabiashara wanaohudhuria kongamano hilo kwa kuiteketeza sayari.
Kongamano hilo la kiuchumi la Davosambalo lilitarajiwa kumalizika siku ya ijumaa, lilitawaliwa na mjadala juu ya mgogoro kati ya Marekani na Ulaya juu ya ruzuku ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi, kuongezeka kwa madeni katika mataifa yanayoendelea pamoja na mizozo mingi ya ulimwengu.