Waliokufa kwa tetemeko Japan wafikia 62
3 Januari 2024Jumatatu alasir tetemeko hilo lenye ukubwa wa kipimo cha 7.6 lilipiga eno la Noto, kuzisambaratisha nyumba na kusababisha ugumu wa kufikisha misaada ya kiutu yenye kuhitajika sana katika maeneo ya mbali ya taifa hilo.
Mvua kubwa imetabiriwa katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo Jumatano hii na hivyo kuongeza hofu ya maporomoko ya ardhi. Taarifa hiyo imezusha hofu kwa juhudi za serikali katika kuwanusuru watu wengi ambao wamenasa kwenye vifusi.
Athari za tetemeko bado kitendawili hadi sasa
Barabara zimeharibika vibaya, miundombinu imebomoka, na maeneo ya mbali ambayo yameathirika vibaya imekuwa vigumu kufikika na kufanikisha juhudi za uokozi. Hadi wakati huu taarifa kamili za athari zilizotokea bado hazijaweza kufahamika ikiwa ni takribani siku mbili baada ya kutokea balaa hilo.
Kwa mfano huko Suzu, mji wenye zaidi ya kaya 5,000 ulio karibu na kitovu cha tetemeko, mamlaka zimeshindwa kujibu miito takriban 72 ya msaada, kwa mujibu wa meya wake Masuhiro Izumiya. Hadi wakati huu mamlaka ilithibitisha vifo 62, kutoka idadi ya awali ya watu 55 ambayo ilitangazwa Jumanne, takwimu ambazo zinalifanya tetemeko hilo kuingia katika rekodi mbaya zaidi tangu 2016.
Kauli ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida alisema "Imekuwa zaidi ya saa 40 tangu tetemeko la kwanza kutokea. Hii ni vita dhidi ya wakati, na ninaamini sasa ni wakati muhimu sana wa vita hivyo." Alikuwa akitoa taarifa baada kikao cha kukabiliana na maafa nchini humo.
Serikali imefungua njia ya bahari kupeleka misaada na baadhi malori makubwa sasa yanaweza kufikia katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi.
Mitsuru Kida mwenye umri wa miaka 74, manusura wa tetemeko la ardhi anayeishi Jiji la Wajima lenye hali ngumu, anaonesha hofu ya kwamba kurejea kwa maisha ya kawaida katika maeneo yake utakuwa mchakato wa muda mrefu.
Soma zaidi:Tsunami yaipiga Japan
Mwaka 2011, nchi hiyo kwa upande wa kaskazini/mashariki ilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi la ukubwa wa 9.0 katika kipimo cha Richter, ambalo lilisababisha tsunami iliyosababisha vifo vya takriban watu 18,500.
Chanzo: RTR