ICJ kutangaza uwezo wake katika kesi ya kuvamiwa Ukraine
2 Februari 2024Katika uamuzi wa awali mnamo Machi 2022, mahakama hiyo ilikubaliana na Ukraine na kuitaka Urusi isitishe uvamizi wake mara moja. Ila Urusi iliupinga uamuzi huo ikisema, mahakama hiyo ambayo jukumu lake ni kuamua mizozo baina ya mataifa, haina uwezo wa kisheria wa kutoa uamuzi katika kesi hiyo.
Urusi pia iliendelea na uvamizi wake na kuonyesha kwa mara nyengine tena, ugumu uliopo kwa mahakama hiyo kutoa hukumu yake ambayo inastahili kuzifunga nchi kisheria.
Ukraine ilifungua kesi siku mbili baada ya uvamizi
Katika kikao cha kusikiliza kesi hiyo mwezi Septemba, mwakilishi wa Ukraine katika mahakama hiyo Anton Korynevych, alidai kwamba "hatua ya Urusi kukiuka maagizo ya mahakama hiyo ni shambulizi kwake pia."
"Kila kombora inalorusha Urusi katika miji yetu, inalirusha kwa kukiuka maagizo ya mahakama hii," alisema Korynevych akiwa amesimama kizimbani, mita chache tu kutoka kwa wapinzani wake katika mahakama hiyo ya ICJ.
Ukraine iliipeleka Urusi katika mahakama hiyo ya haki siku chache tu baada ya kuanza kwa uvamizi huo, ikitaka kukabiliana na jirani yake katika kila hatua, kisheria pamoja na kidiplomasia na kijeshi.
Rais Vladimir Putin alipoagiza kuvamiwa kwa Ukraine mnamo Februari 24, 2022, mojawapo ya sababu zake ilikuwa ni kwamba watu wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine, walikuwa "wanateswa na kufanyiwa mauaji ya kimbari na serikali ya Kyiv."
Siku mbili baadae, Kyiv ilifungua mashtaka ICJ ikipinga vikali sababu hiyo ya Putin na kudai kwamba, hatua ya Urusi kutumia neno "mauaji ya kimbari" imekwenda kinyume na Makubaliano ya mwaka 1948 ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na Mauaji ya Kimbari.
Marekani ilikataliwa kujumuishwa kwenye kesi
Wakili wa Urusi katika kesi hiyo Gennady Kuzmin katika kikao cha mwezi Septemba, alipinga hoja ya Ukraine kwamba Urusi imekwenda kinyume na Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya Umoja wa Mataifa, akisema "huo ni uongo mtupu."
Marafiki 32 wa Ukraine waliiunga mkono Kyiv ila mahakama ya ICJ ililitupilia mbali ombi la Marekani kujumuishwa katika kesi hiyo.
Hapo Jumatano, mahakama ya ICJ ilitoa uamuzi katika kesi nyengine ya Ukraine dhidi ya Urusi, iliyodai kwamba Moscow iliwafadhili waasi waliokuwa wanataka kujitenga mashariki mwa Ukraine kwa miaka kadhaa, kabla kufanya uvamizi wake.
Mahakama hiyo iliyapinga pakubwa madai ya Ukraine na kudai kwamba Urusi ilishindwa tu kuchunguza uwezekano wa kukiukwa sheria ya kufadhili ugaidi.
Vyanzo: AFPE/Reuters