1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

IAEA yaelezea wasiwasi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran

27 Februari 2024

Shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia IAEA limeelezea wasiwasi unaoongezeka kuhusu uwezo wa Iran wa kutengeneza silaza za nyuklia

https://p.dw.com/p/4cwQN
Mkuu wa shirika la IAEA, Rafael Grossi akiwahutubia waandishi habari baada ya mkutano wa bodi ya shirika hilo mjini Vienna nchini Austria Novemba 22, 2023
Mkuu wa shirika la IAEA, Rafael Grossi Picha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Msuguano kati ya Iran na shirika la IAEA umezuka na kukolea mara kwa mara tangu mkataba wa mwaka 2015 ulionuiwa kudhibiti mpango wa nyuklia wa serikali ya mjini Tehran kwa mabadilishano na nafuu ya vikwazo ulipowekwa kapuni.

Soma pia:IAEA: Iran haiko wazi katika mpango wake wa nyuklia

Katika ripoti hiyo mkuu wa shirika la IAEA, Rafael Grossi alisema kauli za wazi hadharani zilizotolewa nchini Iran kuhusu uwezo wa kiufundi wa kutengeneza silaha za nyuklia, zimeongeza wasiwasi kuhusu usahihi na ukamilifu wa matangazo kuhusu hatua za kiusalama zilizotolewa na Iran.

Iran imepunguza ushirikiano na IAEA

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imepunguza ushirikiano na IAEA, kwa kuzima vifaa vya kufuatilia mpango huo wa nyuklia na kuwazuia wakaguzi wa shirika hilo miongoni mwa hatua nyingine.

Soma pia:IAEA yamezuiwa kufika maeneo ya kiwanda cha Zaporizhzhia

Kabla ya mkutano wa bodi ya magavana wa IAEA wiki ijayo, Grossi amesisitiza wito wake kwa Iran kushirikiana kikamilifu na taasisi hiyo na kuongeza kwamba ni kupitia ushirikiano thabiti na wa maana ndipo masuala hayo yanaweza kushughulikiwa.

Picha ya kinu cha nyuklia cha Bushehr Kusini mwa Iran iliyochukuliwa mnamo Oktoba 8, 2021
Kinu cha nyuklia cha Bushehr Kusini mwa IranPicha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Chanzo kimoja cha kidiplomasia kimesema kuwa Iran imekanusha kutengeneza silaha za nyuklia, lakini matamshi ya maafisa na wanasiasa kuhusu uwezo wa kiufundi wa nchi hiyo yamedhoofisha uhusiano ambao tayari unayumba.

Makadirio ya Iran ya hifadhi ya urani iliyorutubishwa yamepita kikomo kilichowekwa katika makubaliano ya mwaka 2015

Katika ripoti tofauti ya siri iliyoonekana na shirika la habari la AFP, IAEA imesema kuwa makadirio ya Iran ya hifadhi ya urani iliyorutubishwa yamefikia zaidi ya mara 27 ya kikomo kilichowekwa katika makubaliano ya mwaka 2015.

Hifadhi jumla ya madini ya urani iliyorutubishwa yaIran ilikadiriwa kuwa kilo 5,525.5 kufikia tarehe 10 mwezi Februari hili likiwa ongezeko la kilo 1,038.7 kutoka mwezi Oktoba.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa Iran wa kupunguza kiwango cha ubora wa akiba yake ya madini ya urani, mwanadiplomasia huyo alielezea kuweko kwa uwezekano wa shinikizo za kisiasa na kwamba huenda Iran haitaki kuongeza mvutano.

Soma pia:Mazunguzo ya nyuklia ya Iran yarefushwa

Mwanadiplomasia huyo pia amesema kuwa huenda taifa hilo liko katika makubaliano na mtu fulani akiongeza kuwa Iran bado inazalisha takriban kilo tisa za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha ubora cha hadi asilimia 60 kwa mwezi.

Mataifa ya Magharibi yachukuwa tahadhari dhidi ya machafuko zaidi Mashariki ya Kati

Wakati kuna mvutano mkubwa unaoendelea katika Mashariki ya Kati, Mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichelea kuiwekea shinikizo Iran kwa hofu ya kuchochea mzozo zaidi.

Soma pia:Marekani na Iran kukamilisha mazungumzo juu ya kuzuia mpango wa nyuklia

Bodi ya magavana ya IAEA, imelaani ukosefu wa ushirikiano kutoka Iran wakati nchi hiyo ikikosa kutimiza baadhi ya makubaliano.

Juhudi za kufufua makubaliano ambayo yangeirejesha Marekani katika mkataba huo naIran kuutii, zilisambaratika wakati wa kipindi cha kiangazi cha mwaka 2022.