Marekani na Iran kukamilisha mazungumzo juu ya kuzuia mpango wa nyuklia
11 Novemba 2014Wakiwa katika hatua ya kufuatia miaka kadhaa ya makubaliano ya kuizuwia Iran na mpango wake wa uzalishaji wa nyuklia, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran Waziri Javad Zarif pamoja na Mshauri mwandamizi wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton walikutana leo kwa siku ya pili kwa mazungumzo katika mji mkuu wa Oman. Ingawa hadi sasa hakuna ishara ya makubaliano ya hakika.
Hali ni ya wasiwasi wakati ikikaribia tarehe 24 Novemba, muda uliowekwa ili kupatikana makubalianao ya kusitisha mpango wa nguvu za nyuklia yataondoa wasi wasi katika eneo la mashariki ya kati kuhusu uwezo wa Iran kutengeneza bomu la nyukliya na kuweza kuufufua uchumi wa jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Pia hatua hiyo itakuwa ni ushindi wa Ikulu ya marekani wa sera yake ya kigeni, ambayo inakosolewa na maseneta wengi wa chama cha Republican na hasa kuhusiana na vita vya Syria na kuongezeka kwa harakati za kundi la Dola la Kiislamu-IS nchini Iraq. Wakosoaji hao hao wanaazma ya kuzuwia mazungumzo katib ya Marekani na Iran, ama kuyavunja kabisa.
Maseneta warepublican kutokuwa na matarajio na Obama kuiweza Iran
Seneta John Mcain wa Arizona amesema utawala wa Obama unapaswa kufahamu kwamba utawala wa iran haujali tena kuhusu marekani na una lengo la kuwaondoa katika mashariki ya kati badala ya kushirikiana nao. McCain ndiye atakaye kuwa mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kijeshi ya baraza la Seneti.
Obama kwa upande wake alikiambia kituo cha mtangazo cha CBS katika kipindi chake cha " Likabili taifa" kwamba vikwazo vilivyowekwa na utawala wake ambavyo havikutarajiwa na iran, ndivyo vilivyolifanya taifa hilo la uajemi likubali kuzungumza. Obama aliongeza kwamba kipa umbele nambari moja kuhusiana na Iran ni kuhakikisha haiundi bomu la nyukliya. Lakini pia rais huyo wa marekani alidokeza juu ya pengo lilioko kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani wakati zikijaribu kufikia makubaliano ya mwisho, akionya " huenda tusifanikiwe kufika huko."
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita , wajumbe wa chama cha Republican katika bunge la Marekani-Kongresi- wameeleza wazi kutokuwa na matarajio yoyote kwamba Obama atafanikiwa katika mkakati wake wa kuijongelea Iran. Wasi wasi wao mkubwa ni kwamba Iran itaendelea kisiri siri kurutubisha madini ya urani kwa lengo la kuunda silaha za nyukliya.
Muda wa zaidi ya tarehe Januari 3 hata hivyo, na ikiwa hadi hapo hakuna makubaliano yatakayofikiwa, huenda bunge la Marekani likajaribu kuweka vikwazo vipya bila ya kumpa nafasi Obama kuvisitisha au kuviondoa. Tayari kuna mpango unaoandaliwa ikiwa mazungumzo yatafikia muda uliowekwa bila ya makubaliano na suala hilo tayari limeshapata uungaji mkono wa maseneta kutoka vyama vyote viwili Democratic na Republican.
Utawala wa Obama unaweza kutumia kura yake ya turufu dhidi ya sheria yoyote ya vikwazo vipya dhidi ya Iran. utawala huo unaamini vikwazo vipya vinaweza kuhujumu masharti ya majadiliano na kusababisha Iran kuimarisha harakati zake za urutubishaji wa urani.
Iran yalilia kuinuliwa kwa vikwazo
Kwa upande wao maafisa wa Iran wanaonekana kwa tahadhari kuwa na matumaini ya kufikiwa makubaliano ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba, lakini wanashikilia vikwazo viondolewe haraka. Wakati wa kipindi hiki cha majadiliano, Iran imekubali kuzuwia hatua yake ya urutubishaji wa urani na kupunguza shehena ya vifaa vinavyohusiana na utengenezaji wa silaha ya nyukliya.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Zarif, amesema vikwazo lazima viondolewe, akiongeza , tangu hapo havijaleta matokeo yoyote ya maana.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ Mohammed Abdul-Rahman, ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman