HRW: Tanzania izingatie haki za binadamu kabla ya uchaguzi
16 Oktoba 2024Taarifa iliyotolewa Jumatano na shirika hilo, imeeleza kuwa tangu mwezi Juni mamlaka imekuwa ikiwamakata kiholela mamia ya wafuasi ya upinzani, kuzuia mitandao ya kijamii, kupiga marufuku vyombo binafsi vya habari, na imekuwa ikihusishwa na utekaji nyara na mauaji ya kiholela ya wakosoaji wanane wa serikali.
Oryem Nyeko, mtafiti mkuu wa Afrika katika shirika la Human Rights Watch anasema mamlaka Tanzania zimeonyesha kuongezeka kwa kutovumilia uhuru wa kujieleza kwa kuwabana wakosoaji wao, na wapinzani wa kisiasa. Nyeko anasema serikali inapaswa kukomesha haraka wimbi la ukandamizaji au hatari ya kuongezeka kwa mazingira ya kisiasa ambayo tayari yana wasiwasi, kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 2024.
Human Rights Watch imesema mamlaka pia inakabiliana na wale wanaoibua wasiwasi kuhusu kutekwa na kupotea kwa watu. Mwezi Agosti, chama kikuu cha upinzani CHADEMA kilitangaza kufanya maandamano jijini Dar es Salaam kupinga hatua ya serikali kuzembea katika kukemea hali hiyo ya watu kutekwa nyara, hata hivyo polisi waliyapiga marufuku maandamano hayo, wakitishia kuwashughulikia watu watakaoandamana.
Kuwabana wapinzani na vyombo vya habari
Septemba 23, polisi waliwakamata na baadaye kuwaachilia kwa dhamana viongozi wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Tundu Lissu, pamoja na wanachama wengine wa chama hicho, kabla ya maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika.
Mapema mwezi Septemba, Shirika la Uchunguzi la Mitandao la NetBlocks lilithibitisha kuwa Tanzania imezuia upatikanai wa mtandao wa kijamii wa X. Tovuti ya NetBlocks ilizuiwa wakati Watanzania wakijihusisha na mijadala ya mitandao ya kijamii kuhusu upotevu huo.
Oktoba 2, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA, ilisitisha leseni za kuchapisha maudhui ya mtandaoni kwa Mwananchi Communications, wachapishaji wa magazeti ya Kiswahili na Kiingereza, baada ya kuchapisha video ya vibonzo inayoonyesha Rais Samia Suluhu Hassan akitazama taarifa ya habari kuhusu utekaji nyara huo. TCRA ilidai kuwa video hiyo inahatarisha umoja wa kitaifa na amani ya kijamii nchini Tanzania.
Mamlaka zatakiwa kuchukuwa hatua
Human Rights Watch inasema ukandamizaji huu unaakisi hali ya kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020, ambako kulikuwa na kuzorota kwa uhuru wa kujieleza na kujumuika na haki nyingine za binadamu. Mamlaka waliwakamata kiholela viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani, walisimamisha kwa muda vyombo vya habari, walifuatilia mawasiliano ya simu za mkononi na kufungia mitandao ya kijamii.
Nyeko anasema katika wakati huu, mamlaka nchini Tanzania zinapaswa kuchukua hatua za haraka kutetea haki za binaadamu na kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki. Kulingana na Human Rights Watch, Rais Samia anapaswa kuhakikisha uchunguzi wa haraka na usio na upendeleo kuhusu kupotea kwa wakosoaji wake na kukomesha vikwazo vinavyoendelea dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa na vyombo huru vya habari.