Hoja ya Brexit na matokeo ya uchaguzi Uingereza
9 Juni 2017Chama cha Conservative cha May ambacho kimepata idadi kubwa ya viti lakini kukosa wingi bungeni, kiliashiria kwamba kitaweza kutumia haki hiyo kwa wakati huu kufanya jaribio la kwanza la kuunda serikali, lakini bado haijawa dhahiri iwapo ataweza kupata uungaji mkono muhimu ili kufanikisha azma hiyo.
Alipoulizwa kuhusu iwapo mazungumzo ya Brexit yaliyopangwa kuanza, Juni 19 kama yatasogezwa mbele ama la, Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn alikiambia kituo cha televisheni cha Sky News kwamba watalazimika kuendelea na mazungumzo hayo.
"Wanatakiwa kuendelea kwa kuwa kifungu cha 50 kilishavujwa. Serikali itakayokuwa madarakani ndani ya siku 11 itatakiwa kufanya mazungumzo ya Brexit. Mahitaji yetu yako wazi, tunataka Brexit itakayotoa kipaumbele cha ajira. Kwa maana hiyo kitu cha muhimu zaidi ni makubaliano ya biashara na Ulaya na ningedhani suala muhimu kwa bunge lingekuwa ni kupiga kura kukubaliana kwamba raia wa nchi wanachama wa EU wanaweza kubakia Uingereza", alisema Corbyn.
Kwa upande mwingine, Corbyn mwenye sera za mrengo wa kushoto ambaye chama chake kimefanya vizuri kuliko ilivyotarajiwa , amesema ni wazi kwamba chama cha Labour kimeshinda uchaguzi huo, na kumtaka May kuachia madaraka akisema amepoteza kura, ushawishi na hajiamini tena.
Waziri wa zamani wa fedha George Osborne, aliyetimuliwa na May, amekiambia kituo cha televisheni cha ITV News kwamba "ni wazi kwamba kama ameanguka vibaya zaidi ya miaka miwili iliyopita na anaweza kushindwa kuunda serikali, basi nina wasiwasi kama ataweza kusalia kwa muda mrefu kama kiongozi wa Conservative."
Hoja kuhusu kuendelea kwa mazungumzo ya Brexit yatawala.
Kwingineko Barani Ulaya, rais wa umoja wa Ulaya , Donald Tusk ameitaka Uingereza kutochelewesha mazungumzo ya Brexit baada ya uchaguzi kuonyesha kutakuwa na bunge lenye wabunge wengi wa upinzani, na kuonya kwamba muda unakimbia sana katika kufikia makubaliano ya talaka hiyo. "hatujui lini mazungumzo yataanza. Tunachojua ni lini yatakamilika. Fanyeni linalowezekana kuzuia kutofikiwa kwa makubaliano," aliandika Tusk kwenye ukarasa wake wa twitter.
Kamishna wa bajeti wa Umoja wa Ulaya Guenther Oettinger amekiambia kituo cha redio cha Ujerumani kwamba wanahitaji serikali iliyo na uwezo wa kuchukua hatua, ambayo itaweza kukubaliana kuhusu Brexit. Amesema Waingereza wanataka kufanya mazungumzo hayo ya kuondoka, lakini kukiwa na washirika dhaifu kuna hatari kwamba hayatakuwa na tija kwa pande zote.
Amesema "EU iko tayari kwa mazungumzo ya Brexit, lakini masaa ama siku chache zijazo ndizo zitaamua iwapo upande huo mwingine utaweza kuanza majadiliano kwa kuwa bila ya serikali, hakutakuwa na mazungumzo."
Waziri mkuu wa Ufaransa Edouard Philippe amekiambia kituo kimoja cha matangazo cha Ufaransa kwamba "Waingereza wameshaamua. Lakini akisema hadhani kama matokeo hayo yanaweza kuzusha hoja kuhusu Brexit, kwa kuwa tayari Waingereza walishaamua. Amesema uchaguzi una mahusiano ya mbali na Brexit na zaidi kwenye masuala ya ndani ambayo ni pamoja na usalama, akiangazia mashambulizi ya kigaidi ya London na Manchester.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba "Waingereza wameshachagua na kusema kwamba nchi yake iko tayari kwa mashirikiano. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Cheki Bohuslav Sobotka, naye ameandika akimpongeza Corbyn kwa kufanikisha kukipandisha chama cha Labour. Amesema kiongozi huyo wa chama cha Labour ndiye mshindi hasa .
Mwandishi: Lilian Mtono/APE/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman