Mzozo kati ya Israel na Hezbollah watishia kutanuka
29 Julai 2024Miito ya kimataifa yatolea ili kuepusha kuutanua mzozo huo. Marekani imelaani tukio hilo na kusema liliendeshwa na Hezbollah huku wakidhihirisha uungwaji mkono usioyumba kwa usalama wa Israel, lakini ikasisitiza pia kwamba haitopendelea kuona mzozo huo unatanuka.
Ufaransa, Uingereza na Misri zilielezea wasiwasi wao kuhusu kutanuka kwa mzozo huo na kwamba unaweza ukaitumbukiza Mashariki ya Kati katika vita vya kikanda. Watu wawili wameuawa kusini mwa Lebanon katika shambulio la kulipiza kisasi la Israel baada ya vijana 12 wa Israel kuuawa kwa roketi siku ya Jumamosi.
Shambulio hilo la droni la Israel kwenye barabara kati ya Shaqra na mji wa mpaka wa kusini wa Mais al-Jabal, limesababisha vifo vya watu wawili na kuwajeruhi wengine kadhaa akiwemo mtoto mmoja. Haikufahamika mara moja ikiwa waliouawa walikuwa wanachama wa kundi la Hezbollah ambalo limekuwa likilengwa na shambulio hilo.
Soma pia: Israel yaapa kujibu shambulizi la Milima ya Golan
Israel ambayo iliapa kulipa kisasi kufuatia shambulio la siku ya Jumamosi katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la milima ya Golan ambapo vijana 12 waliuawa. Baraza la Usalama wa Taifa la Israel limeipatia idhini serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ya kuamua hatua za kuchukua ili kujibu shambulizi hilo.
Israel yaahidi kuiadhibu Hezbollah bila kusababisha vita kamili Mashariki ya Kati
Maafisa wakuu wa ulinzi wa Israel wamesema wanalenga kuishambulia vikali Hezbollah lakini hawadhamirii kulitumbukiza eneo hilo katika vita kamili huku wakisisitiza kuwa nchi hiyo inajiandaa kwa uwezekano wa siku chache za mapigano. Hata hivyo kundi la Hezbollah walikanusha kuhusika na shambulizi hilo la Jumamosi.
Soma pia: Hezbollah yavurumisha maroketi 100 katika milima ya Golan
Kuongezeka kwa uhasama kati ya Israel na kundi la Hezbollah kumesababisha hali ya taharuki nchini Lebanon na raia wamekuwa na hofu kama anavyoelezea Ugarit Abu Assad:
"Ninahofia matokeo. Tazama hilo lililotokea jana, sasa hebu fikiria iwapo litatokea kesho? Na iwapo halii itasababisha vita kamili kutokea bila shaka itakuwa mbaya sana. Watu wengi watakufa katika kila upande.”
Taharuki hiyo imesababisha pia safari za ndege kuahirishwa ama kufutwa katika uwanja wa kimataifa wa Beirut kutokana na mashirika ya bima kuhofia mashambulizi kwa wakati wowote.
Katika hatua nyingine, wakati vita vya Gaza vikiendelea, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema hapo jana kuwa nchi yake inaweza kuingia Israel kama ilivyowahi kufanya huko Libya na Nagorno-Karabakh.
Erdogan ambaye amekuwa mkosoaji mkali wa mashambulizi ya Israel huko Gaza, aliitoa kauli hiyo wakati wa hotuba ya kusifu sekta ya ulinzi ya Uturuki lakini hakufafanua hata hivyo ni aina gani ya uingiliaji ambao angeliufanya katika mzozo huo. Rais huyo wa Uturuki amesema ni lazima wawe imara ili kuchukua uamuzi wa kuingilia kati vita vya Gaza ili kuizuia Israel kuendelea na "matendo yake ya kipuuzi huko Palestina".
(Vyanzo: Mashirika)