Hamas: Mazungumzo ya kusitisha vita Gaza yaanza tena
6 Desemba 2024Afisa mmoja wa Hamas amesema hivi leo kuwa wapatanishi wa kimataifa kutoka Qatar, Misri na Marekani wameanza tena mazungumzo na kundi hilo la wanamgambo pamoja na Israel.
Bassem Naim, afisa wa tawi ya kisiasa ya Hamas ameliambia shirika la habari la Associated Press nchini Uturuki kwamba ana matumaini kuwa mpango huo wa kusitisha vita vya miezi 14 huko Gaza , unaweza kufikiwa kutokana na juhudi mpya zilizochukuliwa hivi karibuni ili kusitisha mapigano, kuachiliwa kwa mateka wa Israel pamoja na wafungwa wa Kipalestina.
" Ni matumaini yetu kwamba kutokana na mabadiliko hasa nchini Marekani baada ya kuchaguliwa tena Donald Trump, ambaye wakati wa kampeni za uchaguzi alitamka hadharani kuwa atasitisha vita vyote, akiingia ofisini anataka kuona vita vyote vimeisha. Tunatumai kwamba hilo litakuwa mchango mzuri na litasaidia haraka iwezekanavyo kufikiwa kwa makubaliano ya usitishaji wa mapigano huko Gaza," alisema afisa huyo.
Qatar ilisitisha mwezi uliopita ushiriki wake kwenye mazungumzo hayo kutokana na kile ilichosema kuwa pande zote hazikuonyesha nia thabiti ya kutaka kuumaliza mzozo huo ulioanza Oktoba 7 mwaka jana baada ya wanamgambo wa Hamas kuishambulia Israel na kuwaua watu wapatao 1,200.
Mashambulizi ya kijeshi ya Israel yaliyofuata dhidi ya eneo la Gaza tayari yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 44,500 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Hii ikiwa ni kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas.
Hayo yakiarifiwa Israel imeendeleza operesheni zake za kijeshi huko Gaza ambapo kulingana na Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International, shambulio la droni la Israel katika hospitali ya kaskazini mwa Gaza limesababisha vifo vya watu wasiopungua 12 wakiwemo maafisa wa afya na kijana mwenye umri wa miaka 16 aliyekuwa kwenye kiti cha magurudumu.
Siku ya Alhamisi, Shirika hilo lilieleza wazi kuwa Israel inafanya mauaji ya halaiki huko Gaza , shutuma ambazo zilikanushwa vikali na serikali mjini Tel-Aviv ambayo inaendelea kukabiliwa na shinikizo kutokana na vita vyake huko Gaza.
Hofu ya kutokea kwa mzozo mpana Mashariki ya Kati
Jeshi la Israel limetangaza kuwa limefanya mashambulizi ya usiku kucha na kuzilenga njia za magendo zinazotumiwa na Hezbollah kusafirisha silaha kwenye mpaka wa Syria na Lebanon.
Pia, Iran imetangaza kuwa imefanikiwa kurusha satelaiti kubwa angani, azma ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikosolewa na nchi za Magharibi zinazosema kuwa hilo linadhihirisha ufanisi wa mpango wa makombora ya masafa marefu wa Tehran.
Wasiwasi umeongezeka wa kulishuhudia eneo la Mashariki ya Kati likitumbukia kwenye mzozo mpana zaidi kutokana na vita vya Gaza, Lebanon, na hivi sasa huko Syria.
(Vyanzo: AP, Reuters, AFP)