Hakuna ahueni Eritrea mwaka baada ya makubaliano na Ethiopia
9 Julai 2019Kwa miaka mingi, Eritrea iliutumia mzozo wake na Ethiopia kama kisingizio cha kuendeleza sera za ukandamizaji, na wengi walitarajia kwamba baada ya makubaliano ya kumaliza mzozo huo, enzi mpya ya kuheshimu haki za binadamu ingechomoza katika nchi hiyo ya upembe wa Afrika.
Lakini, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya hali ya Eritrea katika Baraza la Umoja Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva mapema mwezi huu, mjumbe wa baraza hilo kwa ajili ya Eritrea Daniela Kravetz alisema raia wa kawaida bado hawajaanza kuyaonja matunda ya amani, na hakuna matumaini kuwa hali hiyo itabadilika haraka.
Kuandikishwa jeshini kwa lazima
Adha kubwa kwa watu wa Eritrea ni sheria inayowalazimisha vijana wote kujiunga na jeshi mara tu wanapomaliza elimu ya sekondari, na hakuna muda unaojulikana ambapo vijana hao hatimaye wanaondoka jeshini na kuishi maisha ya kawaida ya kiraia.
Michaela Wrong ambaye ni mchambuzi wa masuala ya Eritrea anayeishi mjini London, anasema sababu ya kuendeleza sera hizo za kubana uhuru wa watu, ni mkakati wa kuwadhibi.
''Bado tunawaona maelfu ya vijana wakivuka mpaka kinyume cha sheria, wakienda katika kambi za wakimbizi nchini Ethiopia, wakivuka jangwa kukimbilia Israel, wakijitosa katika safari hatari za kuvuka Bahari ya Meditarania.'' Amesema Bi Wrong, na kuongeza kuwa serikali ya Eritrea inaendeleza sheria ya kuwaandikisha vijana jeshini ka lazima, kama njia ya kuwadhibi, ikitumai kuzuia wimbi la kudai mageuzi kama lililoshuhudiwa katika ulimwengu wa kiarabu.
Afwerki anaendelea kung'ang'ania madarakani
Tangu mwaka 1993 Eritrea inatawaliwa kiimla na Rais Isaias Afwerki, ambaye serikali yake inakosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, kuwa inawakamata watu kiholela na kuwaweka kizuizini, kukandamiza uhuru wao wa kuabudu, na kuwaandikisha vijana jeshini kwa kipindi kisicho na ukomo.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Eritrea Daniel Kravetz amesema hivi karibuni alipata taarifa za kuhusu kukamatwa kwa wakristo na waislamu wanapokuwa katika mikusanyiko ya sala mjini Asmara, na kutaifishwa kwa vituo vya afya vinavyomilikiwa na kanisa katoliki, baada ya kanisa hilo kuhimiza mjadala ili kuondoa sababu zinazowafanya vijana wengi kuikimbia nchi yao.
Balozi wa Eritrea katika Umoja wa Mataifa Gerahtu Tesfamichae aliipinga vikali ripoti ya mjumbe wa umoja huo katika baraza la haki za binadamu, akisema ilikuwa na lengo la kuyumbisha usalama wa Eritrea.
afpe