1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiHaiti

Karibu watu 7 wauawa nchini Haiti

27 Agosti 2023

Karibu watu 7 wameuwawa jana Jumamosi baada ya kushambuliwa kwa risasi na genge la wahalifu linalodhibiti kitongoji kilicho kaskazini mwa mji mkuu Port-au-Prince.

https://p.dw.com/p/4VcS0
Mwendesha pikipiki akiwa amewabeba raia wakipita katikati ya moshi wa matairi wakati wa maandamano ya kupinga kukosekana kwa usalama Port-au-Prince
Haiti na hasa mji mkuu Port-au-Prince unakabiliwa na visa vya mauaji ya raia vinavyofanywa na magenge ya wahalifuPicha: Richard Pierrin/AFP

Karibu watu 7 wameuwawa jana Jumamosi baada ya kushambuliwa kwa risasi na genge la wahalifu. Genge hilo linalodhibiti kitongoji kilicho kaskazini mwa mji mkuu Port-au-Prince, liliwauwa watu hao waliokuwa kwenye maandamano yaliyoratibiwa na kiongozi wa Kikristo.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini humo la CARDH idadi ya waliouwawa huenda ikaongezeka. Limesema watu kadhaa wamejeruhiwa na baadhi ya waumini wametekwa nyara.

Video iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, iliwaonyesha watu wasiopungua 100 wengi wao wakiwa wamevalia fulana za njano zinazohusishwa na Mchungaji aitwaye Marco wakitembea kuelekea kitongoji cha Canaan, huku baadhi yao wakiwa wamebeba fimbo na mapanga.

Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo hazijathibitishwa zinaonesha watu wakifyatuliwa risasi mitaani na miili ikiwa imetapakaa.

Magenge ya uhalifu yamelielemea jeshi la polisi nchini Haiti, na wachambuzi wanakadiria kwamba magenge hayo yanadhibiti karibu asilimia 80 ya mji mkuu Port-au-Prince.

Soma Pia: UN: Zaidi ya watu 2,400 wamefariki Haiti