1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres: Warohingya wahusishwe kupata suluhu ya mzozo

25 Agosti 2022

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito kwa serikali ya kijeshi nchini Myanmar kuihusisha jamii ya Rohingya katika mchakato wa kusaka suluhu ya mzozo wa kisiasa unaofukuta nchini humo.

https://p.dw.com/p/4G09Z
Türkei | Besuch Antonio Guterres in Istanbul
Picha: Khalil Hamra/AP Photo/picture alliance

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito huo katika mkesha wa maadhimisho ya miaka mitano tangu jamii ya walio wachache ya Waislamu ya Rohingya walipoanza kuhama kwa idadi kubwa kwenda Bangladesh, wakikimbia ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na jeshi katika jimbo la Rakhine kaskazini mwa Myanmar.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Guterres amesisitiza kuhusu kuhusishwa kwa jamii ya Rohingya inayokabiliwa na ubaguzi katika taifa la Myanmar lenye idadi kubwa ya waumini wa Buddha. Wengi wao wananyimwa haki ya uraia na haki nyingine za msingi.

Mzozo huo wa muda mrefu na Warohingya ulianza Agosti 25, 2017 wakati jeshi la Myanmar lilipoanzisha kile ilichokiita kampeni ya safishasafisha katika jimbo la Rakhine, wakijibu mashambulizi yaliyofanywa na makundi ya wanamgambo kwenye vituo vya polisi na walinzi wa mipakani.

Zaidi ya Warohingya 700,000 walikimbilia Bangladesh wakati wanajeshi wa Myanmar wakidaiwa kufanya ubakaji, mauaji pamoja na kuchoma moto maelfu ya makazi.

Januari 2020, Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ iliiagiza Myanmar kufanya kila linalowezekana kuzuia mauaji ya halaiki dhidi ya Warohingya. Siku mbili kabla ya tamko hilo, tume huru iliyoundwa na serikali ya Myanmarilihitimisha kwamba kulikuwa na sababu ya kuamini kwamba vikosi vya usalama vilifanya uhalifu wa kivita dhidi ya jamii hiyo, lakini si mauaji ya halaiki.

Bangladesch Myanmar Grenze Rohingya Flucht Genozid
Raia wa Rohingya wakiwa wamezuiliwa kwenye mpaka wa Rohingya. Wanaharakati wa haki za binaadamu wanasema watu hao wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi, hususan uraia.Picha: YE AUNG THU/AFP

Machi 2022, Marekani ilisema ukandamizaji wa Warohingya ulikuwa ni sawa na mauaji ya halaiki baada ya mamlaka kuthibitisha kuhusu visa vya ukatili mkubwa dhidi ya raia vilivyofanywa na jeshi la Myanmar.

Soma Zaidi: Marekani yasema jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya halaiki

Msemaji wa Guterres amesema wahusika wa uhalifu wote wa kimataifa uliofanywa Myanmar wanatakiwa kuwajibishwa na kuongeza kuwa haki kwa wahanga itasaidia kupatikana kwa mustakabali endelevu na utakaojumuisha watu wote nchini humo.

Mapema mwezi huu, waziri mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina alimwambia mkuu wa shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet kwamba kiasi wakimbizi milioni moja wa Rohingya wanaoishi kwenye makambi yaliyofurika nchini humo wanatakiwa kurejea kwao.

Hata hivyo Dujarric amesema hakuna sababu ya kuwaharakisha akisisitiza kwamba zaidi ya Warohingya 150,000 bado wanazuiwa kwenye makambi katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

Soma Zaidi: Umoja wa Mataifa: Wakimbizi wa Rohingya hawawezi kurudi Myanmar

Serikali ya kijeshi ya Myanmar ilichukua madaraka Februari 2021 baada ya kuipindua serikali iliyochaguliwa na kukabiliwa na upinzani mkubwa wa umma. Wakosoaji wa serikali hiyo wanaituhumu kwa kukiuka kwa kiasi kikubwa haki za binaadamu, matamshi yanayoungwa mkono na Dujarric anayesema hali ya haki za binaadamu na usalama kwa pamoja vimedorora sana nchini Myanmar.

Mashirika: APE