1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ataka wanaozuiliwa Venezuela waachiwe

Josephat Charo
11 Januari 2025

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ameapishwa Ijumaa (10.01.2025) kwa muhula wa tatu wa miaka sita licha ya jumuiya ya kimataifa kukosoa kuchaguliwa kwake tena ikisema ushindi wake sio halali.

https://p.dw.com/p/4p2gL
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: William Volcov/ZUMA Press Wire/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitaka mamlaka za Venezuela kuwaachia huru watu wote waliokamatwa na wanaoednelea kuzuiliwa bila kufunguliwa mashitaka, tangu uchaguzi wa Jula mwaka jana. Msemaji wa Guterres, Stephenie Dujarric amesema katibu mkuu huyo amelaani kuzuiliwa kwa idadi kubwa ya watu wakiwemo viongozi wa upinzani, waandishi habari na watetezi wa haki za binadamu tangu uchaguzi wa rais uliofanyika Julai 28 mwaka uliopita.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amempongeza Maduro kwa kuapishwa kwa awamu ya tatu madarakani. Spika wa bunge la chini la Urusi Vyacheslav Volodin, aliyehudhuria shughuli ya kuapishwa Maduro mjini Caracas kwa niaba ya Putin amewasilisha ujumbe wa pongezi kutoka kwa mkuu huyo wa dola la Urusi.

Kuapishwa kwa Maduro kumekosolewa na kulaaniwa na upinzani wa Venezuela na kuibua kauli za ukosoaji kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. Upinzani unasema kuapishwa kwa Maduro si halali.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizostawi kiviwanda duniani za G7 wamelaani kile walichokiita kuwa ni ukosefu wa uhalali wa demokrasia katika uapisho wa rais Maduro. Katika taaria iliyotolewa na Canada, ambayo ni mwenyekiti wa G7 mwaka huu, mawaziri hao wamekataa ukandamizaji na unga'anga'nizi wa madaraka unaoendelea bila kujali masilahi ya raia wa Venezuela.

Soma pia: Upinzani waapa kuchafua shughuli ya kuapishwa Maduro

Maduro, ambaye amekuwa rais tangu mwaka 2013, alitangazwa na tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Venezuela na Mahakama ya Juu kama mshindi katika uchaguzi uliofanyika mwezi Julai. Hata hivyo, idadi ya kura zinazothibitisha ushindi wake hazijawahi kuchapishwa.

Marekani haimtambui Maduro kama rais wa Venezuela

Marekani imesema haitambui kuchaguliwa kwa Maduro kama rais wa Venezuela na imeahidi tena kutoa dola milioni 25 kwa kukamatwa kwake kuhusiana na mashitka ya kufanya biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Wizara ya mambo ya nje imesema katika taarifa kwamba imeongeza zawadi hiyo hadi kufikia kima hicho kwa taarifa zitakazosaidia kukamatwa rais Maduro pamoja na waziri wa mambo ya ndani Diosdado Cabello.

Nicholas Maduro, kulia, na mke wake, Cilia Flores, wakitabasamu baada ya kuapishwa kwa muhula wa tatu kama rais wa Venezuela
Nicholas Maduro, kulia, na mke wake, Cilia Flores, wakitabasamu baada ya kuapishwa kwa muhula wa tatu kama rais wa VenezuelaPicha: Andres Gonzalez/dpa/picture alliance

Kufuatia kuapishwa kwa Maduro, utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umesema jana Ijumaa kwamba wahamiaji karibu milioni moja kutoka El Salvador, Sudan, Ukraine na Venezuela wataruhusiwa kuendelea kubaki Marekani kwa miezi mingine 18. Hadhi hii hutolewa na wizara ya mambo ya ndani kwa raia wa kigeni ambao hawawezi kurejea kwao kwa sababu ya vita, majanga ya asili au mazingira magumu yasiyo ya kawaida.

Venezuela yawekewa vikwazo

Serikali ya Marekani imeweka vikwazo vipya dhidi ya maafisa wa vyeo vya juu wa Venezuela, saa chache baada ya kuapishwa kwa Maduro. Kwa mujibu wa wizara ya fedha ya Marekani, maafisa wanane walioathiriwa na vikazo hivyo wanawajumuisha mkuu wa kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali Héctor Obregón Pérez, na mkuu wa shirika la ndege la taifa Conviasa, Ramón Celestino Velásquez Araguayán.

Canada, Uingereza na Umoja wa Ulaya pia zimetangaza vikwazo vipya kwa raia wa Venezuela. Uingereza imewawekea vikwazo raia 15 wa Venezuela wenye mafungamano na Maduro, wakiwemo maafisa wa jeshi na majaji. Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimewawekea vikwazo raia wengine 15 wa tume ya kitaifa ya uchaguzi ya Venezuela, idara ya mahakama na maafisa wa usalama wa taifa.

Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Maria Corina Machado amefutilia mbali uwezekano wa kurejea kwa hasimu wa Maduro, kiongozi wa upinzani aliyegombea urais anayeishi kwa sasa uhamishoni, Edmundo Gonzalez. Akizungumza jana baada ya Maduro kuapishwa, Machado alisema si wakati muafaka kwa Gonzalez kurejea nyumbani Venezuela.

(afp, reuters, dpa)