Maduro kuapishwa kwa muhula wa tatu madarakani
10 Januari 2025Kuapishwa kwa Maduro kumegubigwa na maandamano, kutekwa na kuachiwa huru kwa kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado. Machado ndiye kiongozi mashuhuri kabisa wa upinzani ambaye alizuiwa asishiriki uchaguzi wa 2024. Alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza jana tangu alipokwenda mafichoni mwezi Agosti mwaka uliopita.
Vyama vya upinzani nchini Venezuela pamoja na wafuasi wao walifanya maandamano kote nchini jana Alhamisi katika jitihada ya dakika za lala salama kumshinikiza rais Maduro, siku moja kabla kuapishwa kwa muhula wa tatu madarakani.
Marekani imetaka udhalilishaji na mateso yanayofanyiwa viongozi wa upinzani wa Venezuela na rais Maduro na washirika wake yakome. Msemaji wa ikulu ya Marekani amesema katika taarifa kwamba Marekani inaendelea kulaani waziwazi hatua ya Maduro na washirika wake kuutisha upinzani wa kidemokrasia wa Venezuela, muda mfupi baada ya vuguvugu la Machado kusema alikuwa ameachiwa huru baada ya kuzuiwa kwa muda mfupi.
Rais mteule wa Marekani Donald Trump amewatetea watu walioshiriki maandamano ya kumpinga rais Maduro, akisema katika taarifa aliyoituma kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba wapigania uhuru hao wa Venezuela hawatakiwi kudhuriwa.
Kukamatwa kwa Machado kwakosolewa
Kutekwa kwa Machado kuliibua ukosoaji ulimwenguni kote huku serikali ya Colombia ikielezea wasiwasi wake mkubwa na imepinga ongezeko na uzito wa ripoti za matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu yanaoendelea Venezuela kuelekea kuapishwa kwa Maduro.
Wizara ya mambo ya nje ya Uhispania ilisema katika taarifa yake inalaani vikali kukamatwa kwa Machado. Ilisema uadilifu wa kimwili na uhuru wa kujieleza na kuandamana, hususan wa viongozi wa vyama vya kisiasa, lazima ulindwe.
Rais wa Argentina Javier Milei kwa upande wake alikosoa kukamatwa kwa Machado na kuelezea wasiwasi wake kwa shambulizi hilo la kihalifu lililofanywa na utawala wa Maduro. Afisi ya rais Milei ilisema Machado alikamatwa wakati aliposhiriki maandamano halali katika operesheni ya udikteta mbaya kabisa katika historia, ambapo mawakala wa utawala wa Maduro uliwashambulia kwa risasi walinzi wa Machado na kumteka nyara mbele ya maalfu ya waandamanaji.
Marekani ilikanusha madai ya maafisa wa Venezuela kwamba inapanga kumpindua rais Maduro kabla kuapishwa kwa muhula wa tatu kama rais wa Venezuela. Maafisa wa Venezuela walidai kuwa maafisa waandamizi wa vyeo vya juu wa shirika la upelelezi la Marekani FBI na maafisa wa jeshi la Marekani ni miongoni mwa mamluki saba waliokamatwa siku ya Jumanne wiki hii. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema madai yoyote ya Marekani kuhusika katika njama ya kumpindua Maduro ni uongo kabisa.
Ukamataji wa wapinzani Venezuela waibua wasiwasi
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu ukamataji kiholela wa wapinzani nchini Venezuela kabla kuapishwa kwa Maduro. Mkuu wa umoja huo anayeshughulikia masuala ya haki Volker Turk amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu ukamataji huo na kutishwa kwa wapinzani akisema sasa ni wakati wa kupunguza hali ya wasiwasi na kitisho cha machafuko zaidi na kwamba mdahalo ni muhimu.
Akizungumza kabla kuapishwa kwa Maduro hivi leo, Turk alisisitiza kwamba kila mtu ana haki ya uhuru wa kukusanyika kwa amani, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa maoni bila kuingiliwa.
Soma pia: Upinzani waapa kuchafua shughuli ya kuapishwa Maduro
Upinzani na chama tawala Venezuela wanazozana kuhusua matokeo ya uchaguzi wa mwaka uliopita ambao pande zote mbili zinasema zilishinda. Mamlaka inayosimamia uchaguzi nchini humo inasema Maduro alishinda uchaguzi huo uliofanyika mwezi Julai, ingawa hawajawahi kuchapisha majumuisho ya kina ya matokeo.
Serikali ya Venezuela, ambayo imeulaumu upinzani kwa kuchochea njama za kifashisti dhidi yake, imesema itamtia mbaroni kiongozi wa upinzani Edmundo Gonzalez ikiwa atarejea nchini na imewakamata viongozi mashuhuri wa upinzani na wanaharakati kuelekea hafla ya kuapishwa kwa Maduro hivi leo.
Upinzani unasema Gonzalez, mwenye umri wa miaka 75, alishinda kwa kishindo uchaguzi na umeshachapisha matokeo yake kama ushahidi, na hivyo kuungwa mkono na serikali mbalimbali kote ulimwenguni, ikiwemo Marekani inayomchukulia Gonzalez kama rais mteule wa Venezuela.
(afpe, reuteres, ap)