Guterres "asikitishwa" na mauwaji Myanmar
19 Machi 2024Mapigano yametikisa jimbo la Rakhine magharibi mwa Myanmar tangu wapiganaji wa Arakan (AA) waliposhambulia vikosi vya usalama mnamo Novemba, na kumaliza usitishaji mapigano uliodumu kwa kiasi kikubwa tangu mapinduzi ya kijeshi ya 2021.
Guterres amesikitishwa na ripoti za mashambulizi ya anga yanayoendelea kufanywa na jeshi, ikiwa ni pamoja na shambulizi jengine usiku wa Jumatatu katika mji wa Minbya ambako raia wengi waliuwawa na wengine kujeruhiwa.
Mji wa Minbya uko mashariki mwa mji mkuu wa jimbo la Sittwe, ambao umekatizwa na wapiganaji wa AA katika wiki za hivi karibuni.
Soma pia: Vijana wakimbia Myanmar kuepuka kujiunga na jeshi
Kulingana na mkaazi mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama, shambulio hilo la anga lilipiga kijiji cha Thar Dar Jumatatu usiku na kuwaua wanaume 10, wanawake wanne na watoto 10.
Mkazi mwingine ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema watu 23 wameuawa katika mlipuko huo na wengine 18 kujeruhiwa.
Athari za mzozo
Tangu kuibuka tena kwa mzozo huu maelfu ya watu wameyahama makazi yao huko Rakhine, ambapo ukandamizaji wa kijeshi wa 2017 ulipelekea maelfu ya Warohingya kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.
Jeshi la Myanmar limekuwa na udhibiti katika mji wa Sittwe lakini katika wiki za hivi karibuni wapiganaji wa AA wamepata mafanikio katika wilaya jirani.
Aidha mapigano pia yameenea hadi nchi jirani za India na Bangladesh.
Mwezi uliopita, takriban watu wawili waliuawa nchini Bangladesh baada ya makombora yaliyorushwa kutoka Myanmar wakati wa mapigano kuvuka mpaka.
AA ni moja ya makundi yenye silaha kutoka makabila kadhaa ya watu wachache katika maeneo ya mpakani mwa Myanmar, ambao wengi wao wamepigana na jeshi tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1948 kuhusu uhuru na udhibiti wa rasilimali.