1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia na purukushani zaigubika Libya

21 Februari 2011

Nchini Libya,maandamano ya kudai demokrasia yameingia siku yake ya saba na kiasi ya watu 200 wameuawa katika ghasia hizo.

https://p.dw.com/p/10L5o
Ramani ya Libya

Wakati huohuo,mtoto wa kiume wa kiongozi wa Libya,Saif al-Islam Kadhaffi ametahadharisha kuwa uwezekano wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokea upo endapo waandamanaji hawatouitikia wito wa serikali.Kwa upande mwengine,Umoja wa Ulaya unasubiriwa kutoa kauli yake kuhusu hali hiyo.

Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa vituo viwili vya televisheni vilitiwa moto jana usiku pamoja na afisi za bunge zilizoko katikati ya mji mkuu wa Tripoli.

Unruhen in Libyen Flash-Galerie
Waandamanaji wa Benghazi,LibyaPicha: AP

Vita vya wenyewe kwa wenye

Akizungumza kwenye kituo cha televisheni mapema hii leo (21.02.2011),Saif al-Islam Kadhafi alitahadharisha na kutisha kuwa endapo waandamanaji hao hawatakikubali inachosema serikali,uwezekano wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokea upo mkubwa kwani serikali itapambana nao mpaka dakika ya mwisho.Saif al-islam Kadhafi alizilaani harakati hizo za wanadamanaji wanaompinga babake,Kanali Muammar Gaddafi,ambaye amekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 41.Alikiri kuwa makosa yalitendeka wakati maafisa wa usalama walipopambana na waandamanaji hao ila anaamini kuwa mataifa ya kigeni yana mkono wake katika hali hiyo kwa jumla.  

Wakati huohuo,takwimu za Shirika la Kutetea Haki za binadamu Human Rights Watch zinaeleza kuwa kiasi ya watu 233 wameuawa tangu ghasia hizo zianze Alhamisi iliyopita.

Kulingana na mwandishi wa habari wa shirika la AFP,milio mingi ya risasi imesikika kwa mara ya kwanza katika mji mkuu wa Tripoli tangu ghasia zianze.

EU Außenministerin Catherine Ashton EU zu Libyen
Catherine Ashton kabla ya kikao cha dharura kuhusu LibyaPicha: AP

Yote hayo yakiendelea,kundi la kiasi ya watu 500 raia wa Libya walikivamia kiwanda kimoja cha Korea Kusini kilicho karibu na mji mkuu wa Libya.Tukio hilo liliwajeruhi wafanyakazi 15 wa Bangladesh na watatu wa Korea Kusini kama zilivyoeleza duru za mambo ya kigeni za Korea Kusini.

Mapigano yanaripotiwa kutokea katika uwanja wa Kijani ulio katikati ya mji ambako waandamanaji walipambana na wafuasi wa kiongozi wa Libya Kanali Muammara Gaddafi.Purukushani hizo zilianzia Jumanne iliyopita katika mji wa Benghazi na kuenea hadi Misrata ulio karibu na Tripoli.Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia iliyo na ushirikiano mkubwa wa kibiashara na Libya anasisitiza kuwa wanaifuatilia hali hiyo kwa karibu na,"Kama mujuavyo Italia ndiyo nchi iliyo karibu zaidi na Libya na Tunisia.Kwahiyo tunatiwa wasiwasi na athari za hali hiyo hususan katika masuala ya uhamiaji kwenye eneo lililo kusini mwa bahari ya Mediterranea." 

NO FLASH Italien Lampedusa Immigranten aus Nordafrika
Wahamiaji haramu wakiwasili Lampedusa:Italia inalazimika kutumia mbinu maalum kuwazuiaPicha: AP

Vitisho na uhamiaji

Kwa upande wake Libya imetishia kuwa itausitisha ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya katika suala la kuudhibiti uhamiaji.Itakumbukwa kuwa maelfu ya raia wa eneo hilo la Maghreb walikivamia kisiwa cha Italia cha Lampedusa kwasababu ya purukushani zilizotokea hivi karibuni.

Kwa upande mwengine,Waziri Mkuu wa Libya Baghdadi Mahmudi aliwaeleza mabalozi wa Umoja wa Ulaya kuwa kuna mipango maalum iliyo na misingi yake kwenye ugaidi iliyo na azma ya kuigeuza Libya kuwa ngome ya ugaidi.Hata hivyo,uongozi wa Libya unaelekea kukabiliwa na mpasuko baada ya balozi wake katika Umoja wa Mataifa ya Kiarabu,Arab League,Abdel Moneim al-Honi kutangaza kuwa anajiunga na harakati hizo za kuipinga serikali.Mabalozi wa Libya katika nchi za China na India nao pia wamejiuzulu kwasababu ya hali iliyoko nchini mwao.  

Libya ni mshirika mkuu

Jamii ya kimataifa imevilaani vikali vitendo vya uongozi wa Libya vya kutumia nguvu ili kuwasambaratisha waandamanaji hao.Ili kuupa msukumo msimamo wao,mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kutoa kauli yao hii leo inayoikosoa serikali ya Libya kwasababu ya kuwazuwia wanaharakati hao.Mkuu wa sera za kigeni wa Jumuiya hiyo Catherine Ashton anasisitiza kuwa la msingi ni kuyasikiliza matakwa ya raia na anajiandaa kuizuri Misri ambako,"ziara hiyo itanipa fursa zaidi ya kuyasikiliza wanayoyasema raia wa eneo hilo kadhalika jinsi tutakavyoweza kuwasaidia wanapojiandaa kurejea katika mfumo wa demokrasia.Tunatoa wito wa kujizuwia,kusitisha ghasia na kuyapa umuhimu majadiliano,"alieleza. 

Saif al-Islam Gaddafi Konferenz
Saif al-Islam Gaddafi,mwanawe Kanali Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Haki ya msingi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameutolea wito uongozi wa Libya kutotumia nguvu vilevile kuuheshimu uhuru wa waandamanaji hao ambao ni haki ya msingi.Mawaziri hao wanakutana mjini Brussels ili kuijadili hali nzima kwa jumla katika eneo la Maghreb na mataifa ya Kiarabu.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman