1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la ghadhabu lapiga katika ulimwengu wa kiarabu

18 Februari 2011

Maandamano yanaendelea leo katika baadhi ya nchi za mashariki ya kati na Afrika kaskazini, ambapo wananchi wanatoa joto lao la roho dhidi ya serikali zao nchini Bahrein,Yemen, Libya na Misri.

https://p.dw.com/p/10JRY
Muammar Ghaddafi atikisika?Picha: AP

Maelfu ya wanaharakati wanaodai mageuzi wameshaanza kuteremka majiani katika mji wa mashariki ya Libya-Benghazi mapema hii leo-siku moja baada ya "siku ya ghadhabu" iliyosababisha kwa mujibu wa shirika linalopigania haki za binaadamu, Human Rights Watch, watu wasiopungua 24 kupoteza maisha yao juzi na jana. Wanajeshi wamejazana majiani katika mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Libya.

Flash-Galerie Unruhen Proteste in Nahost Bahrain
Mazishi ya mhanga mmojawapo wa machafuko ya jana mjini ManamaPicha: AP

Nchini Bahrain wanajeshi wanapiga doria pia mjini Manama baada ya polisi hapo jana kufyetua gesi za kutoa machozi kuwatimua mamia ya waandamanaji toka uwanja mkuu wa Lulu. Maelfu ya waandamanaji wanahudhuria hii leo mazishi ya wahanga wawili waliouliwa jana na huku wakipaza sauti na kusema:"Si shia na wala si Sunni."Umoja wa taifa" au Washiya na wasunni ni ndugu."Kuna wanaohanikiza pia wakisema "Umma unataka utawala ung'oke madarakani."

Hasira za washia wa Bahrein zinaweza kuwaambukiza wenzao walio wachache katika nchi jirani ya Saud Arabia, nchi inayosafirisha mafuta kwa wingi duniani.

Machafuko katika eneo hilo yamepelekea bei ya mafuta ghafi kupanda na kufikia dala 104 kwa pipa na ndio chanzo pia cha kuzidi kuoengezeka bei ya dhahabu duniani.

Jumuia ya kimataifa imewasihi viongozi wa serikali katika nchi zote hizo zinazokumbwa na ghadhabu ya umma wasikilize kilio cha wananchi wao. Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-Moon, amesema:

"Kwa kujibu maandamano ya amani, viongozi wanawajibika kuheshimu haki za binaadam.Wasitumie nguvu kokote kule. Ninawahimiza wote wajizuwie.Umoja wa mataifa unawahimiza viongozi wa eneo hilo na kote kwengine ulimwenguni wawasikilize kwa makini wananchi wao na wajibu matakwa yao ya haki."

Ägypten Großkundgebung auf dem Tahrir-Patz in Kairo
Waandamanaji wakusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini CairoPicha: AP

Nchini Yemen watu watatu wameuwawa jana usiku kufuatia machafuko kati ya waandamanani na vikosi vya polisi katika mji wa kusini wa Aden.

Maandamano yanaendelea katika miji kadhaa ya Yemen kati ya wafuasi na wapinzani wa rais Ali Abadallah Saleh.

Na hatimae nchini Misri waandalizi wa vuguvugu la mageuzi wanategemea zaidi ya watu milioni moja watashiriki hii leo baada ya sala ya ijumaa katika maandamano ya ushindi-wiki moja baada ya kuondoka madarakani Hosni Mubarak. Vikosi vya usalama vimewekwa kuepusha machafuko.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/Afp

Mpitiaji.Miraji Othman