GENEVA: Shirika la afya duniani laandaa mkutano wa siku tatu mjini Geneva
7 Novemba 2005Shirika la afya duniani, WHO, limeanza mkutano wa siku tatu mjini Geneva Uswissi, pamoja na benki kuu ya dunia, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, na mashirika yanayohusika na afya ya mifugo. Mkutano huo unalenga kutafuta mbinu za kuchangisha na kutawanya fedha za kupambana na homa ya ndege.
Benki ya dunia inasema homa ya binadamu ambayo inaweza kusababishwa na aina hiyo hatari ya homa ya ndege inaweza kuyagharimu mataifa yaliyoendelea kiviwanda kiasi cha dola bilioni 550. Katika ripoti yake juu ya homa hiyo ya ndege, benki hiyo imesema, kuzuka kwa ugonjwa huo huenda kukasababisha vifo kati ya eflu 100 na elfu 200 nchini Marekani pekee, ambavyo imesema vitasababisha hasara ya kati ya dola bilioni 100 na bilioni 200.
Hii leo virusi wanaosababisha homa ya ndege aina ya H5N1 wamegunduliwa kwenye ndege aliyekuwa amekufa huko nchini Russia.