Gavana ashambuliwa siku chache kabla ya uchaguzi Nigeria
14 Februari 2019Wakati huo huo, chama kikuu cha upinzani cha Nigeria kimedai kwamba tume ya uchaguzi imekuwa na zaidi ya wapiga kura milioni moja hewa katika daftari la wapiga kura.
Wanachama wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu la kanda ya Afrika Magharibi wamedai kuhusika na shambulio la jana dhidi ya msafara wa Kashim Shettima, gavana wa jimbo la kaskazini mashariki la Borno, na kusababisha watu 42 kuuwawa: Hayo ni kwa mujibu wa kundi linalofanya utafiti wa kijasusi la marekani SITE Intel.
Ofisi ya Shettima, ambayo msafara wake ulishambuliwa wakati wa mkutano wa kampeni karibu na mji wa Dikwa, kabla ya uchaguzi utakaofanyika nchi nzima Februari 16, hata hivyo imethibitisha kuuwawa kwa watu watatu.
Mjumbe wa kundi la walinzi wa umma katika eneo hilo, lililoudwa ili kulinda vijiji katika jimbo la Borno dhidi ya ugaidi, amesema watu kadhaa wamekamatwa wakati wa shambulio hilo la kushitukiza.
"Raia wawili pamoja na mwanajeshi mmoja waliuwawa papo hapo, wakati watu wenye silaha waliondoka na magari manane," aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwa masharti ya kutotajwa jina.
"Baadhi ya watu katika msafara huo waliwakamatwa mateka na kuondoka nao," ameongeza.
Ukaguzi wa daftari ya wapiga kura
Wakati huo huo mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Peoples Democratic Party, PDP Uche Secondus, amesema katika mkutano na waandishi habari mjini Abuja kwamba tume ya uchaguzi nchini humo, haikufanya ukaguzi wa daftari la wapiga kura, kabla ya kuchapisha majina ya wapiga kura.
"Maelezo ambayo si mazuri yamejitokeza, moja kati ya njia za wizi wa kura , ni kutoweka rekdi halisi ya daftari ya wapiga kura na kwa hiyo si rahisi kuamini ukuaji wa demokrasi na taifa kwa jumla, amesema mwenyekiti huyo.
Pia amedai kwamba kulikuwa na utaratibu ulioratibiwa wa kuandikisha watu wa mataifa ya kigeni kuwa wapiga kura katika uchaguzi huo.
Chama cha Peoples Democratic Party, ambacho mgombea wake wa kiti cha urais ni Atiku Abubakar, ni chama kikuu cha upinzani nchini Nigeria. Madai ya wapiga kura hewa yanaelekea kuzusha wasi wasi katika kile ambacho kinaonekana kuwa ni mpambano utakaotoa matokeo ya karibu kati ya Abubakar, makamu wa rais wa zamani , na rais Muhammadu Buhari.
Tume ya uchaguzi imesema watu milioni 84 wameandikishwa kupiga kura katika nchi hiyo yenye wakaazi milioni 190.
Msemaji wa tume ya uchaguzi hakupatikana kutoa maelezo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ap / dpa
Mhariri: Grace Patricia Kabogo