Gambia yamkamata mwandishi kwa madai ya kumchafua rais
27 Septemba 2024Polisi ya Gambia imemkamata mwandishi habari aliyeripoti kwamba rais wa nchi hiyo ana mipango ya kuachia madaraka kuelekea uchaguzi wa mwaka 2026.
Mwandishi hiyo Momodou Darboe alichapisha ripoti kwenye gazeti la The Voice la nchini humo mapema wiki hii iliyodai kwamba Rais Adama Barrow anafanyia kazi mpango wa kuondoka madarakani na amemteua mfanyabiasahra mashuhuri Muhammed Jah kuwa "mrithi wake".
Mawakili wa rais walitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya gazeti hilo wakisema madai yaliyotolewa ni ya kumchafulia jina Rais Barrow na hayana ukweli wowote.
Hata hivyo katika taarifa iliyotolewa leo, polisi imesema imemkamata Darboe na mhariri wa gazeti la The Voice Musa Sheriff. Taarifa hiyo imesema Sheriff ameachiwa kwa dhamana lakini Darboe anafunguliwa mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye makala yake ambayo polisi imesema ilikuwa na lengo la kuzusha hamkani nchini humo.
Kukamatwa kwake kumetokea katika wakati Rais Barrow alitoa hotuba mbele ya Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa jana akijatapa kuwa nchi yake ni miongoni mwa zile zinazoongoza barani Afrika kwa ulinzi wa haki ya watu kujieleza.
Alisema anafarijika kuuambia ulimwengu kwamba tangu mwaka 2017, Gambia haijawahi kuwa na mfungwa yeyote wa kisiasa au mwandishi habari au mtetezi wa haki za binadamu aliyefungwa jela.