1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya awali Gambia Adama Barrow aongoza kwa kura chache

Zainab Aziz Mhariri Saumu Njama
5 Desemba 2021

Rais wa sasa wa Gambia Adama Barrow anaongoza kwa kura chache baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya awali kwenye eneo bunge moja huku kura zikiwa bado zaendelea kuhesabiwa.

https://p.dw.com/p/43quX
Gambia | Präsidentschaftswahlen in Serrekunda
Picha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Gambia Alieu Momarr Njai, aliwaambia waandishi wa habari kwamba matokeo hayo ya awali kutoka kwenye jimbo la kwanza kati ya jumla ya majimbo 53 yalionyesha Barrow akiongoza kwa kura 657 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Ousainou Darboe aliyepata kura 454.

Kushoto: Rais wa Gambia Adama Barrow baada ya kupiga kura yake katika mji wa Banjul
Kushoto: Rais wa Gambia Adama Barrow baada ya kupiga kura yake katika mji wa BanjulPicha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa leo Jumapili kwa kuzingatia mfumo rahisi wa wingi wa kura baada ya kuhesabiwa kutoka kwenye kila eneo bunge.

Gambia inatumia mfumo wa kipekee wa upigaji kura kwa kutumia vipande vya marumaru vinavyotumbukizwa ndani ya debe la kila mgombea ili kuepuka kura kuharibika.

Wananchi wa Gambia walipiga kura hapo jana Jumamosi katika uchaguzi wa kwanza wa rais kwenye taifa hilo dogo la Afrika Magharibi tangu rais wa zamani Yahya Jammeh alipokimbilia uhamishoni.

Rais huyo wa zamani Yahya Jammeh aliondoka madarakani mnamo mwaka 2016 baada ya kushindwa kwenye uchaguzi hatua iliyo umaliza utawala wake wa miaka 22.

Ousainou Darboe wa chama cha UDP, mpinzani mkuu wa Rais Adama Barrow
Ousainou Darboe wa chama cha UDP, mpinzani mkuu wa Rais Adama BarrowPicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Rais wa sasa Adama Barrow anayetetea muhula wa pili mwenye umri wa miaka 56 anashindana na wapinzani watano akiwemo mshauri wake wa kisiasa wa zamani Ousainou Darboe, mwenye umri wa miaka 73, ambaye ndiye mpinzani wake mkuu.

Wagombea wengine ni pamoja na Essa Mbye Faal, ambaye aliwahi kuwa mshauri mkuu wa Tume ya Ukweli, Maridhiano na Fidia nchini Gambia iliyoorodhesha historia ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika utawala wa Yahya Jammeh.  Mwingine ni Mama Kandeh, aliyeshika nafasi ya tatukwenye uchaguzi wa mwaka 2016 ambaye anaungwa mkono na rais wa zamani Yahya Jammeh.

Rais wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh
Rais wa zamani wa Gambia Yahya JammehPicha: picture-alliance/dpa/Taiwan Press Office

Mapema siku ya Jumamosi, Barrow alipiga kura yake katika mji mkuu wa Gambia, Banjul na alisema kwamba alikuwa na uhakika wa kushinda.

Karibu watu milioni 1 kutoka kwenye idadi ya watu milioni 2.5 ndio waliojiandikisha kupiga kura nchini Gambia, ambayo ni nchi ndogo zaidi barani Afrika. Gambia pia ni taifa lenye kiwango kikubwa cha watu wasiojua kusoma na kuandika.

Vyanzo:RTRE/DPA