Naibu wa Rais Kenya akimbilia mahakamani kuzuwia kutimuliwa
3 Oktoba 2024Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kwamba Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua siku ya leo amewasilisha ombi katika mahakama mjini Nairobi akitaka kusitishwa kwa mchakato wa kumuondoa katika nafasi yake ulioanzishwa dhidi yake na wabunge mapema wiki hii.
Washirika wa Rais wa Kenya William Ruto waliwasilisha maombi ya kuondolewa kwa Naibu rais Gachagua siku ya Jumanne wakimshtumu kwa kuchochea chuki za kikabila na kudhoofisha serikali.
Soma pia: Bunge la Kenya lapokea hoja ya kumuondosha makamu wa rais
Gachagua anasema ametengwa na amekanusha shutuma za washirika wa Ruto kwamba alihusika na vurugu maandamano ya vijana maarufu Gen Z dhidi ya serikali mapema mwaka huu.
Katika ombi hilo lililowasilishwa Alhamisi ya leo na Gachagua amesema kuwa hoja ya kumshtaki ilikuwa ni ya "uchochezi wa kisiasa uliopangwa ili kushinda utashi wa uhuru wa watu wa Kenya ulioonyeshwa kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 2022," Gazeti la Star limeripoti.